Surah 21: Al-Anbiya — الأنبياء
ٱقْتَرَبَ لِلنَّاسِ حِسَابُهُمْ وَهُمْ فِى غَفْلَةٍۢ مُّعْرِضُونَ
IMEWAKARIBIA watu hisabu yao, nao wamo katika mghafala wanapuuza.
مَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍۢ مِّن رَّبِّهِم مُّحْدَثٍ إِلَّا ٱسْتَمَعُوهُ وَهُمْ يَلْعَبُونَ
Hayawafikilii mawaidha mapya kutoka kwa Mola wao Mlezi ila huyasikiliza na huku wanafanya mchezo.
لَاهِيَةًۭ قُلُوبُهُمْ ۗ وَأَسَرُّوا۟ ٱلنَّجْوَى ٱلَّذِينَ ظَلَمُوا۟ هَلْ هَٰذَآ إِلَّا بَشَرٌۭ مِّثْلُكُمْ ۖ أَفَتَأْتُونَ ٱلسِّحْرَ وَأَنتُمْ تُبْصِرُونَ
Zimeghafilika nyoyo zao. Na wale walio dhulumu hunong'onezana kwa siri: Ni nani ati huyu isipo kuwa ni binaadamu tu kama nyinyi! Mnauwendea uchawi hali nanyi mnaona?
قَالَ رَبِّى يَعْلَمُ ٱلْقَوْلَ فِى ٱلسَّمَآءِ وَٱلْأَرْضِ ۖ وَهُوَ ٱلسَّمِيعُ ٱلْعَلِيمُ
Alisema: Mola wangu Mlezi anayajua yasemwayo mbinguni na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
بَلْ قَالُوٓا۟ أَضْغَٰثُ أَحْلَٰمٍۭ بَلِ ٱفْتَرَىٰهُ بَلْ هُوَ شَاعِرٌۭ فَلْيَأْتِنَا بِـَٔايَةٍۢ كَمَآ أُرْسِلَ ٱلْأَوَّلُونَ
Lakini wao walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua tu, bali huyo ni mtunga mashairi. Basi atuletee miujiza kama walivyo tumwa wale wa mwanzo.
مَآ ءَامَنَتْ قَبْلَهُم مِّن قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَٰهَآ ۖ أَفَهُمْ يُؤْمِنُونَ
Hawakuamini kabla yao watu wa mji tulio uangamiza. Basi, je, wataamini hawa?
وَمَآ أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ إِلَّا رِجَالًۭا نُّوحِىٓ إِلَيْهِمْ ۖ فَسْـَٔلُوٓا۟ أَهْلَ ٱلذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ
Na kabla yako hatukuwatuma ila watu wanaume tulio wapa wahyi (ufunuo). Basi waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui.
وَمَا جَعَلْنَٰهُمْ جَسَدًۭا لَّا يَأْكُلُونَ ٱلطَّعَامَ وَمَا كَانُوا۟ خَٰلِدِينَ
Wala hatukuwafanya miili isiyo kula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele.
ثُمَّ صَدَقْنَٰهُمُ ٱلْوَعْدَ فَأَنجَيْنَٰهُمْ وَمَن نَّشَآءُ وَأَهْلَكْنَا ٱلْمُسْرِفِينَ
Kisha tukawatimizia miadi, na tukawaokoa wao na tulio wataka, na tukawateketeza walio pita mipaka.
لَقَدْ أَنزَلْنَآ إِلَيْكُمْ كِتَٰبًۭا فِيهِ ذِكْرُكُمْ ۖ أَفَلَا تَعْقِلُونَ
Na hakika tumekuteremshieni Kitabu ambacho ndani yake yamo makumbusho yenu. Je! Hamzingatii?
وَكَمْ قَصَمْنَا مِن قَرْيَةٍۢ كَانَتْ ظَالِمَةًۭ وَأَنشَأْنَا بَعْدَهَا قَوْمًا ءَاخَرِينَ
Na mingapi katika miji iliyo kuwa ikidhulumu tumeiteketeza, na tukawasimamisha baada yao watu wengine.
فَلَمَّآ أَحَسُّوا۟ بَأْسَنَآ إِذَا هُم مِّنْهَا يَرْكُضُونَ
Basi walipo ihisi adhabu yetu, mara wakaanza kukimbia.
لَا تَرْكُضُوا۟ وَٱرْجِعُوٓا۟ إِلَىٰ مَآ أُتْرِفْتُمْ فِيهِ وَمَسَٰكِنِكُمْ لَعَلَّكُمْ تُسْـَٔلُونَ
Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu, na maskani zenu, mpate kusailiwa!
قَالُوا۟ يَٰوَيْلَنَآ إِنَّا كُنَّا ظَٰلِمِينَ
Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhaalimu.
فَمَا زَالَت تِّلْكَ دَعْوَىٰهُمْ حَتَّىٰ جَعَلْنَٰهُمْ حَصِيدًا خَٰمِدِينَ
Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya kama walio fyekwa, wamezimika.
وَمَا خَلَقْنَا ٱلسَّمَآءَ وَٱلْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَٰعِبِينَ
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yao kwa mchezo.
لَوْ أَرَدْنَآ أَن نَّتَّخِذَ لَهْوًۭا لَّٱتَّخَذْنَٰهُ مِن لَّدُنَّآ إِن كُنَّا فَٰعِلِينَ
Kama tungeli taka kufanya mchezo tunge jifanyia Sisi wenyewe, lau kwamba tungeli kuwa ni wafanyao mchezo.
بَلْ نَقْذِفُ بِٱلْحَقِّ عَلَى ٱلْبَٰطِلِ فَيَدْمَغُهُۥ فَإِذَا هُوَ زَاهِقٌۭ ۚ وَلَكُمُ ٱلْوَيْلُ مِمَّا تَصِفُونَ
Bali tunaitupa kweli juu ya uwongo ikauvunja na mara ukatoweka. Na ole wenu kwa mnayo yazua.
وَلَهُۥ مَن فِى ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ ۚ وَمَنْ عِندَهُۥ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِۦ وَلَا يَسْتَحْسِرُونَ
Na ni vyake Yeye tu Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na katika ardhi. Na walioko kwake hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki.
يُسَبِّحُونَ ٱلَّيْلَ وَٱلنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ
Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei.
أَمِ ٱتَّخَذُوٓا۟ ءَالِهَةًۭ مِّنَ ٱلْأَرْضِ هُمْ يُنشِرُونَ
Au wamepata miungu katika ardhi inayo fufua?
لَوْ كَانَ فِيهِمَآ ءَالِهَةٌ إِلَّا ٱللَّهُ لَفَسَدَتَا ۚ فَسُبْحَٰنَ ٱللَّهِ رَبِّ ٱلْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ
Lau wangeli kuwamo humo miungu wengine isipo kuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeli fisidika. Subahana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayo yazua.
لَا يُسْـَٔلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْـَٔلُونَ
Yeye hahojiwi kwa ayatendayo, na wao ndio wanao hojiwa kwa wayatendayo.
أَمِ ٱتَّخَذُوا۟ مِن دُونِهِۦٓ ءَالِهَةًۭ ۖ قُلْ هَاتُوا۟ بُرْهَٰنَكُمْ ۖ هَٰذَا ذِكْرُ مَن مَّعِىَ وَذِكْرُ مَن قَبْلِى ۗ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ٱلْحَقَّ ۖ فَهُم مُّعْرِضُونَ
Au wanawaabudu miungu mingine badala yake? Sema: Leteni ushahidi wenu! Haya ni ukumbusho wa hawa walio nami, na ukumbusho wa walio kabla yangu. Lakini wengi wao hawaijui kweli, na kwa hivyo wanapuuza.
وَمَآ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِىٓ إِلَيْهِ أَنَّهُۥ لَآ إِلَٰهَ إِلَّآ أَنَا۠ فَٱعْبُدُونِ
Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu.
وَقَالُوا۟ ٱتَّخَذَ ٱلرَّحْمَٰنُ وَلَدًۭا ۗ سُبْحَٰنَهُۥ ۚ بَلْ عِبَادٌۭ مُّكْرَمُونَ
Na wanasema: Arrahman, Mwingi wa Rehema, ana mwana! Subhanahu, Ametakasika na hayo! Bali hao (wanao waita wana) ni watumwa walio tukuzwa.
لَا يَسْبِقُونَهُۥ بِٱلْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِۦ يَعْمَلُونَ
Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri zake.
يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ٱرْتَضَىٰ وَهُم مِّنْ خَشْيَتِهِۦ مُشْفِقُونَ
Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawamwombei yeyote ila yule anaye mridhia Yeye, nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea.
۞ وَمَن يَقُلْ مِنْهُمْ إِنِّىٓ إِلَٰهٌۭ مِّن دُونِهِۦ فَذَٰلِكَ نَجْزِيهِ جَهَنَّمَ ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِى ٱلظَّٰلِمِينَ
Na yeyote kati yao atakaye sema: Mimi ni mungu, badala yake, basi huyo tutamlipa malipo yake Jahannamu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wenye kudhulumu.
أَوَلَمْ يَرَ ٱلَّذِينَ كَفَرُوٓا۟ أَنَّ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضَ كَانَتَا رَتْقًۭا فَفَتَقْنَٰهُمَا ۖ وَجَعَلْنَا مِنَ ٱلْمَآءِ كُلَّ شَىْءٍ حَىٍّ ۖ أَفَلَا يُؤْمِنُونَ
Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai? Basi je, hawaamini?
وَجَعَلْنَا فِى ٱلْأَرْضِ رَوَٰسِىَ أَن تَمِيدَ بِهِمْ وَجَعَلْنَا فِيهَا فِجَاجًۭا سُبُلًۭا لَّعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ
Na tukaweka katika ardhi milima iliyo thibiti ili isiwayumbishe, na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka.
وَجَعَلْنَا ٱلسَّمَآءَ سَقْفًۭا مَّحْفُوظًۭا ۖ وَهُمْ عَنْ ءَايَٰتِهَا مُعْرِضُونَ
Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa, lakini wanazipuuza Ishara zake.
وَهُوَ ٱلَّذِى خَلَقَ ٱلَّيْلَ وَٱلنَّهَارَ وَٱلشَّمْسَ وَٱلْقَمَرَ ۖ كُلٌّۭ فِى فَلَكٍۢ يَسْبَحُونَ
Na Yeye ndiye aliye umba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote katika anga vinaogelea.
وَمَا جَعَلْنَا لِبَشَرٍۢ مِّن قَبْلِكَ ٱلْخُلْدَ ۖ أَفَإِي۟ن مِّتَّ فَهُمُ ٱلْخَٰلِدُونَ
Nasi hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako kuwa na maisha ya milele. Basi je! Ukifa wewe, wao wataishi milele?
كُلُّ نَفْسٍۢ ذَآئِقَةُ ٱلْمَوْتِ ۗ وَنَبْلُوكُم بِٱلشَّرِّ وَٱلْخَيْرِ فِتْنَةًۭ ۖ وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ
Kila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa.
وَإِذَا رَءَاكَ ٱلَّذِينَ كَفَرُوٓا۟ إِن يَتَّخِذُونَكَ إِلَّا هُزُوًا أَهَٰذَا ٱلَّذِى يَذْكُرُ ءَالِهَتَكُمْ وَهُم بِذِكْرِ ٱلرَّحْمَٰنِ هُمْ كَٰفِرُونَ
Na wakikuona walio kufuru hawakufanyi wewe ila ni kitu cha maskhara tu, (wakisema): Je! Ndiye huyu anaye itaja miungu yenu? Na hali wao wanakataa kumkumbuka Arrahman, Mwingi wa Rehema!
خُلِقَ ٱلْإِنسَٰنُ مِنْ عَجَلٍۢ ۚ سَأُو۟رِيكُمْ ءَايَٰتِى فَلَا تَسْتَعْجِلُونِ
Mwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni Ishara zangu. Basi msinihimize.
وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَٰذَا ٱلْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَٰدِقِينَ
Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
لَوْ يَعْلَمُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ حِينَ لَا يَكُفُّونَ عَن وُجُوهِهِمُ ٱلنَّارَ وَلَا عَن ظُهُورِهِمْ وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ
Lau wangeli jua wale walio kufuru wakati ambao hawatauzuia Moto kwenye nyuso zao wala migongo yao, na wala hawatanusuriwa!
بَلْ تَأْتِيهِم بَغْتَةًۭ فَتَبْهَتُهُمْ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ رَدَّهَا وَلَا هُمْ يُنظَرُونَ
Bali utawafikia kwa ghafla, na utawashitua na wala hawataweza kuurudisha, wala hawatapewa muhula!
وَلَقَدِ ٱسْتُهْزِئَ بِرُسُلٍۢ مِّن قَبْلِكَ فَحَاقَ بِٱلَّذِينَ سَخِرُوا۟ مِنْهُم مَّا كَانُوا۟ بِهِۦ يَسْتَهْزِءُونَ
Na Mitume walio kabla yako walikwisha dhihakiwa. Kwa hivyo wale walio wafanyia maskhara yaliwafika yale waliyo kuwa wakiyafanyia dhihaka.
قُلْ مَن يَكْلَؤُكُم بِٱلَّيْلِ وَٱلنَّهَارِ مِنَ ٱلرَّحْمَٰنِ ۗ بَلْ هُمْ عَن ذِكْرِ رَبِّهِم مُّعْرِضُونَ
Sema: Nani anaye kulindeni usiku na mchana na Arrahmani Mwingi wa Rehema? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao Mlezi.
أَمْ لَهُمْ ءَالِهَةٌۭ تَمْنَعُهُم مِّن دُونِنَا ۚ لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَ أَنفُسِهِمْ وَلَا هُم مِّنَّا يُصْحَبُونَ
Au wao wanao miungu watao weza kuwakinga nasi? Hao hawawezi kujinusuru nafsi zao, wala hawatalindwa nasi!
بَلْ مَتَّعْنَا هَٰٓؤُلَآءِ وَءَابَآءَهُمْ حَتَّىٰ طَالَ عَلَيْهِمُ ٱلْعُمُرُ ۗ أَفَلَا يَرَوْنَ أَنَّا نَأْتِى ٱلْأَرْضَ نَنقُصُهَا مِنْ أَطْرَافِهَآ ۚ أَفَهُمُ ٱلْغَٰلِبُونَ
Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha zake? Basi je! Hao ni wenye kushinda?
قُلْ إِنَّمَآ أُنذِرُكُم بِٱلْوَحْىِ ۚ وَلَا يَسْمَعُ ٱلصُّمُّ ٱلدُّعَآءَ إِذَا مَا يُنذَرُونَ
Sema: Mimi nakuonyeni kwa Wahyi. Na viziwi hawasikii wito wanapo onywa.
وَلَئِن مَّسَّتْهُمْ نَفْحَةٌۭ مِّنْ عَذَابِ رَبِّكَ لَيَقُولُنَّ يَٰوَيْلَنَآ إِنَّا كُنَّا ظَٰلِمِينَ
Na wanapo guswa na mpulizo mmoja tu wa adhabu itokayo kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka wao husema: Ole wetu! Hakika tulikuwa wenye kudhulumu.
وَنَضَعُ ٱلْمَوَٰزِينَ ٱلْقِسْطَ لِيَوْمِ ٱلْقِيَٰمَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌۭ شَيْـًۭٔا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍۢ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَٰسِبِينَ
Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu.
وَلَقَدْ ءَاتَيْنَا مُوسَىٰ وَهَٰرُونَ ٱلْفُرْقَانَ وَضِيَآءًۭ وَذِكْرًۭا لِّلْمُتَّقِينَ
Na kwa yakini tuliwapa Musa na Haaruni kipambanuzi, na mwangaza, na makumbusho kwa wachamngu,
ٱلَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِٱلْغَيْبِ وَهُم مِّنَ ٱلسَّاعَةِ مُشْفِقُونَ
Ambao wanamkhofu Mola wao Mlezi faraghani, na wanaiogopa Saa ya Kiyama.
وَهَٰذَا ذِكْرٌۭ مُّبَارَكٌ أَنزَلْنَٰهُ ۚ أَفَأَنتُمْ لَهُۥ مُنكِرُونَ
Na haya ni makumbusho yaliyo barikiwa, tuliyo yateremsha. Basi je! Mnayakataa?
۞ وَلَقَدْ ءَاتَيْنَآ إِبْرَٰهِيمَ رُشْدَهُۥ مِن قَبْلُ وَكُنَّا بِهِۦ عَٰلِمِينَ
Na hakika tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu wake zamani, na tulikuwa tunamjua.
إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِۦ مَا هَٰذِهِ ٱلتَّمَاثِيلُ ٱلَّتِىٓ أَنتُمْ لَهَا عَٰكِفُونَ
Alipo mwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu mnayo yashughulikia kuyaabudu?
قَالُوا۟ وَجَدْنَآ ءَابَآءَنَا لَهَا عَٰبِدِينَ
Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu.
قَالَ لَقَدْ كُنتُمْ أَنتُمْ وَءَابَآؤُكُمْ فِى ضَلَٰلٍۢ مُّبِينٍۢ
Akasema: Bila ya shaka nyinyi na baba zenu mmekuwa katika upotofu ulio dhaahiri.
قَالُوٓا۟ أَجِئْتَنَا بِٱلْحَقِّ أَمْ أَنتَ مِنَ ٱللَّٰعِبِينَ
Wakasema: Je! Umetujia kwa maneno ya kweli au wewe ni katika wachezao tu?
قَالَ بَل رَّبُّكُمْ رَبُّ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ ٱلَّذِى فَطَرَهُنَّ وَأَنَا۠ عَلَىٰ ذَٰلِكُم مِّنَ ٱلشَّٰهِدِينَ
Akasema: Bali Mola wenu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ambaye ndiye aliye ziumba. Na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo.
وَتَٱللَّهِ لَأَكِيدَنَّ أَصْنَٰمَكُم بَعْدَ أَن تُوَلُّوا۟ مُدْبِرِينَ
Na Wallahi! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu haya baada ya mkisha geuka kwenda zenu.
فَجَعَلَهُمْ جُذَٰذًا إِلَّا كَبِيرًۭا لَّهُمْ لَعَلَّهُمْ إِلَيْهِ يَرْجِعُونَ
Basi akayavunja vipande vipande, ila kubwa lao, ili wao walirudie.
قَالُوا۟ مَن فَعَلَ هَٰذَا بِـَٔالِهَتِنَآ إِنَّهُۥ لَمِنَ ٱلظَّٰلِمِينَ
Wakasema: Nani aliye ifanyia haya miungu yetu? Hakika huyu ni katika walio dhulumu.
قَالُوا۟ سَمِعْنَا فَتًۭى يَذْكُرُهُمْ يُقَالُ لَهُۥٓ إِبْرَٰهِيمُ
Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim.
قَالُوا۟ فَأْتُوا۟ بِهِۦ عَلَىٰٓ أَعْيُنِ ٱلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَشْهَدُونَ
Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate kumshuhudia!
قَالُوٓا۟ ءَأَنتَ فَعَلْتَ هَٰذَا بِـَٔالِهَتِنَا يَٰٓإِبْرَٰهِيمُ
Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe Ibrahim?
قَالَ بَلْ فَعَلَهُۥ كَبِيرُهُمْ هَٰذَا فَسْـَٔلُوهُمْ إِن كَانُوا۟ يَنطِقُونَ
Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi waulizeni ikiwa wanaweza kutamka.
فَرَجَعُوٓا۟ إِلَىٰٓ أَنفُسِهِمْ فَقَالُوٓا۟ إِنَّكُمْ أَنتُمُ ٱلظَّٰلِمُونَ
Basi wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi mlikuwa madhaalimu!
ثُمَّ نُكِسُوا۟ عَلَىٰ رُءُوسِهِمْ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا هَٰٓؤُلَآءِ يَنطِقُونَ
Kisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao wakasema: Wewe unajua kwamba hawa hawesemi.
قَالَ أَفَتَعْبُدُونَ مِن دُونِ ٱللَّهِ مَا لَا يَنفَعُكُمْ شَيْـًۭٔا وَلَا يَضُرُّكُمْ
Akasema: Basi nyinyi mnawaabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu wasio kufaini kitu wala kukudhuruni?
أُفٍّۢ لَّكُمْ وَلِمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ ٱللَّهِ ۖ أَفَلَا تَعْقِلُونَ
Aibu yenu nyinyi na hivyo mnavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Basi nyinyi hamtii akilini?
قَالُوا۟ حَرِّقُوهُ وَٱنصُرُوٓا۟ ءَالِهَتَكُمْ إِن كُنتُمْ فَٰعِلِينَ
Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo!
قُلْنَا يَٰنَارُ كُونِى بَرْدًۭا وَسَلَٰمًا عَلَىٰٓ إِبْرَٰهِيمَ
Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim!
وَأَرَادُوا۟ بِهِۦ كَيْدًۭا فَجَعَلْنَٰهُمُ ٱلْأَخْسَرِينَ
Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio walio khasiri.
وَنَجَّيْنَٰهُ وَلُوطًا إِلَى ٱلْأَرْضِ ٱلَّتِى بَٰرَكْنَا فِيهَا لِلْعَٰلَمِينَ
Na tukamwokoa yeye na Luut'i tukawapeleka kwenye nchi tulio ibariki kwa ajili ya walimwengu wote.
وَوَهَبْنَا لَهُۥٓ إِسْحَٰقَ وَيَعْقُوبَ نَافِلَةًۭ ۖ وَكُلًّۭا جَعَلْنَا صَٰلِحِينَ
Naye tukampa Is-haq, na Yaaqub kuwa ni ziada. Na wote tukawajaalia wawe watu wema.
وَجَعَلْنَٰهُمْ أَئِمَّةًۭ يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا وَأَوْحَيْنَآ إِلَيْهِمْ فِعْلَ ٱلْخَيْرَٰتِ وَإِقَامَ ٱلصَّلَوٰةِ وَإِيتَآءَ ٱلزَّكَوٰةِ ۖ وَكَانُوا۟ لَنَا عَٰبِدِينَ
Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.
وَلُوطًا ءَاتَيْنَٰهُ حُكْمًۭا وَعِلْمًۭا وَنَجَّيْنَٰهُ مِنَ ٱلْقَرْيَةِ ٱلَّتِى كَانَت تَّعْمَلُ ٱلْخَبَٰٓئِثَ ۗ إِنَّهُمْ كَانُوا۟ قَوْمَ سَوْءٍۢ فَٰسِقِينَ
Na Luut'i tukampa hukumu na ilimu na tukamwokoa na ule mji ulio kuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wachafu.
وَأَدْخَلْنَٰهُ فِى رَحْمَتِنَآ ۖ إِنَّهُۥ مِنَ ٱلصَّٰلِحِينَ
Na tukamuingiza katika rehema yetu. Hakika yeye ni miongoni mwa watenda mema.
وَنُوحًا إِذْ نَادَىٰ مِن قَبْلُ فَٱسْتَجَبْنَا لَهُۥ فَنَجَّيْنَٰهُ وَأَهْلَهُۥ مِنَ ٱلْكَرْبِ ٱلْعَظِيمِ
Na Nuhu alipo ita zamani, nasi tukamuitikia, na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa.
وَنَصَرْنَٰهُ مِنَ ٱلْقَوْمِ ٱلَّذِينَ كَذَّبُوا۟ بِـَٔايَٰتِنَآ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا۟ قَوْمَ سَوْءٍۢ فَأَغْرَقْنَٰهُمْ أَجْمَعِينَ
Na tukamnusuru na watu walio zikanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawazamisha wote.
وَدَاوُۥدَ وَسُلَيْمَٰنَ إِذْ يَحْكُمَانِ فِى ٱلْحَرْثِ إِذْ نَفَشَتْ فِيهِ غَنَمُ ٱلْقَوْمِ وَكُنَّا لِحُكْمِهِمْ شَٰهِدِينَ
Na Daud na Suleiman walipo kata hukumu katika kadhiya ya konde walipo lisha humo mbuzi wa watu usiku. Na Sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao hiyo.
فَفَهَّمْنَٰهَا سُلَيْمَٰنَ ۚ وَكُلًّا ءَاتَيْنَا حُكْمًۭا وَعِلْمًۭا ۚ وَسَخَّرْنَا مَعَ دَاوُۥدَ ٱلْجِبَالَ يُسَبِّحْنَ وَٱلطَّيْرَ ۚ وَكُنَّا فَٰعِلِينَ
Tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa hukumu na ilimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tulio fanya hayo.
وَعَلَّمْنَٰهُ صَنْعَةَ لَبُوسٍۢ لَّكُمْ لِتُحْصِنَكُم مِّنۢ بَأْسِكُمْ ۖ فَهَلْ أَنتُمْ شَٰكِرُونَ
Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru?
وَلِسُلَيْمَٰنَ ٱلرِّيحَ عَاصِفَةًۭ تَجْرِى بِأَمْرِهِۦٓ إِلَى ٱلْأَرْضِ ٱلَّتِى بَٰرَكْنَا فِيهَا ۚ وَكُنَّا بِكُلِّ شَىْءٍ عَٰلِمِينَ
Na tukamsahilishia Suleiman upepo wa kimbunga wendao kwa amri yake kwenye ardhi tuliyo ibarikia. Na Sisi ndio tunao jua kila kitu.
وَمِنَ ٱلشَّيَٰطِينِ مَن يَغُوصُونَ لَهُۥ وَيَعْمَلُونَ عَمَلًۭا دُونَ ذَٰلِكَ ۖ وَكُنَّا لَهُمْ حَٰفِظِينَ
Na pia mashet'ani wanao mpigia mbizi na kufanya kazi nyenginezo. Na Sisi tulikuwa walinzi wao.
۞ وَأَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُۥٓ أَنِّى مَسَّنِىَ ٱلضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ ٱلرَّٰحِمِينَ
Na Ayyubu, alipo mwita Mola wake Mlezi, akasema: Mimi yamenipata madhara. Na Wewe ndiye unaye rehemu kuliko wote wanao rehemu.
فَٱسْتَجَبْنَا لَهُۥ فَكَشَفْنَا مَا بِهِۦ مِن ضُرٍّۢ ۖ وَءَاتَيْنَٰهُ أَهْلَهُۥ وَمِثْلَهُم مَّعَهُمْ رَحْمَةًۭ مِّنْ عِندِنَا وَذِكْرَىٰ لِلْعَٰبِدِينَ
Basi tukamwitikia, na tukamwondolea madhara aliyo kuwa nayo, na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema inayo toka kwetu, na ukumbusho kwa wafanyao ibada.
وَإِسْمَٰعِيلَ وَإِدْرِيسَ وَذَا ٱلْكِفْلِ ۖ كُلٌّۭ مِّنَ ٱلصَّٰبِرِينَ
Na Ismail, na Idris, na Dhulkifli - wote walikuwa miongoni mwa wanao subiri.
وَأَدْخَلْنَٰهُمْ فِى رَحْمَتِنَآ ۖ إِنَّهُم مِّنَ ٱلصَّٰلِحِينَ
Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao walikuwa katika watu wema.
وَذَا ٱلنُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَٰضِبًۭا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِى ٱلظُّلُمَٰتِ أَن لَّآ إِلَٰهَ إِلَّآ أَنتَ سُبْحَٰنَكَ إِنِّى كُنتُ مِنَ ٱلظَّٰلِمِينَ
Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: Hapana mungu isipo kuwa Wewe Subhanaka Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.
فَٱسْتَجَبْنَا لَهُۥ وَنَجَّيْنَٰهُ مِنَ ٱلْغَمِّ ۚ وَكَذَٰلِكَ نُۨجِى ٱلْمُؤْمِنِينَ
Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na hivyo ndivyo tunavyo waokoa Waumini.
وَزَكَرِيَّآ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُۥ رَبِّ لَا تَذَرْنِى فَرْدًۭا وَأَنتَ خَيْرُ ٱلْوَٰرِثِينَ
Na Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi: Mola wangu Mlezi! Usiniache peke yangu, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi.
فَٱسْتَجَبْنَا لَهُۥ وَوَهَبْنَا لَهُۥ يَحْيَىٰ وَأَصْلَحْنَا لَهُۥ زَوْجَهُۥٓ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا۟ يُسَٰرِعُونَ فِى ٱلْخَيْرَٰتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًۭا وَرَهَبًۭا ۖ وَكَانُوا۟ لَنَا خَٰشِعِينَ
Basi tukamwitikia, na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe. Hakika wao walikuwa wepesi wa kutenda mema, na wakituomba kwa shauku na khofu. Nao walikuwa wakitunyenyekea.
وَٱلَّتِىٓ أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا فَنَفَخْنَا فِيهَا مِن رُّوحِنَا وَجَعَلْنَٰهَا وَٱبْنَهَآ ءَايَةًۭ لِّلْعَٰلَمِينَ
Na mwanamke aliye linda uke wake, na tukampulizia katika roho yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni Ishara kwa walimwengu.
إِنَّ هَٰذِهِۦٓ أُمَّتُكُمْ أُمَّةًۭ وَٰحِدَةًۭ وَأَنَا۠ رَبُّكُمْ فَٱعْبُدُونِ
Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.
وَتَقَطَّعُوٓا۟ أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ ۖ كُلٌّ إِلَيْنَا رَٰجِعُونَ
Nao wakalikata jambo lao hili mapande mapande baina yao. Wote watarudi kwetu.
فَمَن يَعْمَلْ مِنَ ٱلصَّٰلِحَٰتِ وَهُوَ مُؤْمِنٌۭ فَلَا كُفْرَانَ لِسَعْيِهِۦ وَإِنَّا لَهُۥ كَٰتِبُونَ
Na atendaye mema naye ni Muumini basi haitakataliwa juhudi yake. Na hakika Sisi tunamwandikia.
وَحَرَٰمٌ عَلَىٰ قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَٰهَآ أَنَّهُمْ لَا يَرْجِعُونَ
Na haiwi kwa wana-mji tulio uangamiza, ya kwamba hawatarejea,
حَتَّىٰٓ إِذَا فُتِحَتْ يَأْجُوجُ وَمَأْجُوجُ وَهُم مِّن كُلِّ حَدَبٍۢ يَنسِلُونَ
Mpaka watapo funguliwa Juju na Maajuju wakawa wanateremka kutoka kila mlima;
وَٱقْتَرَبَ ٱلْوَعْدُ ٱلْحَقُّ فَإِذَا هِىَ شَٰخِصَةٌ أَبْصَٰرُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ يَٰوَيْلَنَا قَدْ كُنَّا فِى غَفْلَةٍۢ مِّنْ هَٰذَا بَلْ كُنَّا ظَٰلِمِينَ
Na miadi ya haki ikakaribia. Hapo ndipo yatapo kodoka macho ya walio kufuru (na watasema:) Ole wetu! Bila ya shaka tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu.
إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ ٱللَّهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَٰرِدُونَ
Hakika nyinyi na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu.
لَوْ كَانَ هَٰٓؤُلَآءِ ءَالِهَةًۭ مَّا وَرَدُوهَا ۖ وَكُلٌّۭ فِيهَا خَٰلِدُونَ
Lau kuwa hawa ni miungu, wasingeli ingia. Na wote watadumu humo.
لَهُمْ فِيهَا زَفِيرٌۭ وَهُمْ فِيهَا لَا يَسْمَعُونَ
Lao wao humo ni kupiga mayowe, na wala hawatasikia (jenginelo).
إِنَّ ٱلَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا ٱلْحُسْنَىٰٓ أُو۟لَٰٓئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ
Ama wale ambao wema wetu umewatangulia, hao watatenganishwa na hayo.
لَا يَسْمَعُونَ حَسِيسَهَا ۖ وَهُمْ فِى مَا ٱشْتَهَتْ أَنفُسُهُمْ خَٰلِدُونَ
Hawatausikia mvumo wake, na wao watadumu katika yale zinayo yatamani nafsi zao.
لَا يَحْزُنُهُمُ ٱلْفَزَعُ ٱلْأَكْبَرُ وَتَتَلَقَّىٰهُمُ ٱلْمَلَٰٓئِكَةُ هَٰذَا يَوْمُكُمُ ٱلَّذِى كُنتُمْ تُوعَدُونَ
Hicho Kitisho Kikubwa hakito wahuzunisha. Na Malaika watawapokea (kwa kuwaambia): Hii ndiyo Siku yenu mliyo kuwa mkiahidiwa!
يَوْمَ نَطْوِى ٱلسَّمَآءَ كَطَىِّ ٱلسِّجِلِّ لِلْكُتُبِ ۚ كَمَا بَدَأْنَآ أَوَّلَ خَلْقٍۢ نُّعِيدُهُۥ ۚ وَعْدًا عَلَيْنَآ ۚ إِنَّا كُنَّا فَٰعِلِينَ
Siku tutakapo zikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyo anza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao.
وَلَقَدْ كَتَبْنَا فِى ٱلزَّبُورِ مِنۢ بَعْدِ ٱلذِّكْرِ أَنَّ ٱلْأَرْضَ يَرِثُهَا عِبَادِىَ ٱلصَّٰلِحُونَ
Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema.
إِنَّ فِى هَٰذَا لَبَلَٰغًۭا لِّقَوْمٍ عَٰبِدِينَ
Hakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao ibada.
وَمَآ أَرْسَلْنَٰكَ إِلَّا رَحْمَةًۭ لِّلْعَٰلَمِينَ
Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.
قُلْ إِنَّمَا يُوحَىٰٓ إِلَىَّ أَنَّمَآ إِلَٰهُكُمْ إِلَٰهٌۭ وَٰحِدٌۭ ۖ فَهَلْ أَنتُم مُّسْلِمُونَ
Sema: Hakika imefunuliwa kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Je! Mmesilimu?
فَإِن تَوَلَّوْا۟ فَقُلْ ءَاذَنتُكُمْ عَلَىٰ سَوَآءٍۢ ۖ وَإِنْ أَدْرِىٓ أَقَرِيبٌ أَم بَعِيدٌۭ مَّا تُوعَدُونَ
Na kama wakigeuka, basi sema: Nimekutangazieni sawa sawa, wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyo ahidiwa.
إِنَّهُۥ يَعْلَمُ ٱلْجَهْرَ مِنَ ٱلْقَوْلِ وَيَعْلَمُ مَا تَكْتُمُونَ
Hakika Yeye anajua kauli ya dhaahiri na anajua myafichayo.
وَإِنْ أَدْرِى لَعَلَّهُۥ فِتْنَةٌۭ لَّكُمْ وَمَتَٰعٌ إِلَىٰ حِينٍۢ
Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo.
قَٰلَ رَبِّ ٱحْكُم بِٱلْحَقِّ ۗ وَرَبُّنَا ٱلرَّحْمَٰنُ ٱلْمُسْتَعَانُ عَلَىٰ مَا تَصِفُونَ
Sema: Mola wangu Mlezi! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu Mlezi ni Mwingi wa Rehema, aombwaye msaada juu ya mnayo yazua.
Surah 22: Al-Hajj — الحج
يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ ٱتَّقُوا۟ رَبَّكُمْ ۚ إِنَّ زَلْزَلَةَ ٱلسَّاعَةِ شَىْءٌ عَظِيمٌۭ
Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi. Hakika tetemeko la Saa (ya Kiyama) ni jambo kuu.
يَوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّآ أَرْضَعَتْ وَتَضَعُ كُلُّ ذَاتِ حَمْلٍ حَمْلَهَا وَتَرَى ٱلنَّاسَ سُكَٰرَىٰ وَمَا هُم بِسُكَٰرَىٰ وَلَٰكِنَّ عَذَابَ ٱللَّهِ شَدِيدٌۭ
Siku mtapo iona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba ataharibu mimba yake. Na utaona watu wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.
وَمِنَ ٱلنَّاسِ مَن يُجَٰدِلُ فِى ٱللَّهِ بِغَيْرِ عِلْمٍۢ وَيَتَّبِعُ كُلَّ شَيْطَٰنٍۢ مَّرِيدٍۢ
Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, na wanamfuata kila shet'ani aliye asi.
كُتِبَ عَلَيْهِ أَنَّهُۥ مَن تَوَلَّاهُ فَأَنَّهُۥ يُضِلُّهُۥ وَيَهْدِيهِ إِلَىٰ عَذَابِ ٱلسَّعِيرِ
Ameandikiwa kwamba anaye mfanya kuwa rafiki, basi huyo hakika atampoteza na atamwongoza kwenye adhabu ya Moto mkali.
يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ إِن كُنتُمْ فِى رَيْبٍۢ مِّنَ ٱلْبَعْثِ فَإِنَّا خَلَقْنَٰكُم مِّن تُرَابٍۢ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍۢ ثُمَّ مِنْ عَلَقَةٍۢ ثُمَّ مِن مُّضْغَةٍۢ مُّخَلَّقَةٍۢ وَغَيْرِ مُخَلَّقَةٍۢ لِّنُبَيِّنَ لَكُمْ ۚ وَنُقِرُّ فِى ٱلْأَرْحَامِ مَا نَشَآءُ إِلَىٰٓ أَجَلٍۢ مُّسَمًّۭى ثُمَّ نُخْرِجُكُمْ طِفْلًۭا ثُمَّ لِتَبْلُغُوٓا۟ أَشُدَّكُمْ ۖ وَمِنكُم مَّن يُتَوَفَّىٰ وَمِنكُم مَّن يُرَدُّ إِلَىٰٓ أَرْذَلِ ٱلْعُمُرِ لِكَيْلَا يَعْلَمَ مِنۢ بَعْدِ عِلْمٍۢ شَيْـًۭٔا ۚ وَتَرَى ٱلْأَرْضَ هَامِدَةًۭ فَإِذَآ أَنزَلْنَا عَلَيْهَا ٱلْمَآءَ ٱهْتَزَّتْ وَرَبَتْ وَأَنۢبَتَتْ مِن كُلِّ زَوْجٍۭ بَهِيجٍۢ
Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kufufuliwa basi kwa hakika Sisi tulikuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana na kipande cha damu ilio gandana, kisha kutokana na kipande cha nyama chenye umbo na kisicho kuwa na umbo, ili tukubainishieni. Nasi tunakiweka katika matumbo ya uzazi tunacho kitaka mpaka muda ulio wekwa. Kisha tunakutoeni kwa hali ya mtoto mchanga, kisha mfikie kutimia akili. Na wapo katika nyinyi wanao kufa, na wapo katika nyinyi wanao rudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa, hata mtu awe hajui kitu baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapo yateremsha maji juu yake husisimka na kututumka, na kumea kila namna ya mimea mizuri.
ذَٰلِكَ بِأَنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلْحَقُّ وَأَنَّهُۥ يُحْىِ ٱلْمَوْتَىٰ وَأَنَّهُۥ عَلَىٰ كُلِّ شَىْءٍۢ قَدِيرٌۭ
Hayo ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki, na kwamba hakika Yeye ndiye mwenye kuhuisha wafu, na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.
وَأَنَّ ٱلسَّاعَةَ ءَاتِيَةٌۭ لَّا رَيْبَ فِيهَا وَأَنَّ ٱللَّهَ يَبْعَثُ مَن فِى ٱلْقُبُورِ
Na kwamba hakika Saa itakuja hapana shaka kwa hilo, na kwamba hakika Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini.
وَمِنَ ٱلنَّاسِ مَن يُجَٰدِلُ فِى ٱللَّهِ بِغَيْرِ عِلْمٍۢ وَلَا هُدًۭى وَلَا كِتَٰبٍۢ مُّنِيرٍۢ
Na katika watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru.
ثَانِىَ عِطْفِهِۦ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ ٱللَّهِ ۖ لَهُۥ فِى ٱلدُّنْيَا خِزْىٌۭ ۖ وَنُذِيقُهُۥ يَوْمَ ٱلْقِيَٰمَةِ عَذَابَ ٱلْحَرِيقِ
Anaye geuza shingo yake ili kupoteza watu waache Njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha adhabu ya kuungua.
ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ يَدَاكَ وَأَنَّ ٱللَّهَ لَيْسَ بِظَلَّٰمٍۢ لِّلْعَبِيدِ
(Ataambiwa): Hayo ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yako. Na hakika Mwenyezi Mungu si dhaalimu kwa waja.
وَمِنَ ٱلنَّاسِ مَن يَعْبُدُ ٱللَّهَ عَلَىٰ حَرْفٍۢ ۖ فَإِنْ أَصَابَهُۥ خَيْرٌ ٱطْمَأَنَّ بِهِۦ ۖ وَإِنْ أَصَابَتْهُ فِتْنَةٌ ٱنقَلَبَ عَلَىٰ وَجْهِهِۦ خَسِرَ ٱلدُّنْيَا وَٱلْءَاخِرَةَ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ ٱلْخُسْرَانُ ٱلْمُبِينُ
Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni. Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amekhasiri dunia na Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi.
يَدْعُوا۟ مِن دُونِ ٱللَّهِ مَا لَا يَضُرُّهُۥ وَمَا لَا يَنفَعُهُۥ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ ٱلضَّلَٰلُ ٱلْبَعِيدُ
Badala ya Mwenyezi Mungu, yeye huomba kisicho mdhuru wala kumnufaisha. Huko ndiko kupotolea mbali!
يَدْعُوا۟ لَمَن ضَرُّهُۥٓ أَقْرَبُ مِن نَّفْعِهِۦ ۚ لَبِئْسَ ٱلْمَوْلَىٰ وَلَبِئْسَ ٱلْعَشِيرُ
Humuomba yule ambaye bila ya shaka dhara yake ipo karibu zaidi kuliko nafuu yake. Kwa hakika huyo ni mlinzi muovu, na rafiki muovu.
إِنَّ ٱللَّهَ يُدْخِلُ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّٰلِحَٰتِ جَنَّٰتٍۢ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَٰرُ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ
Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema katika Bustani zipitazo mito kati yake. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda atakayo.
مَن كَانَ يَظُنُّ أَن لَّن يَنصُرَهُ ٱللَّهُ فِى ٱلدُّنْيَا وَٱلْءَاخِرَةِ فَلْيَمْدُدْ بِسَبَبٍ إِلَى ٱلسَّمَآءِ ثُمَّ لْيَقْطَعْ فَلْيَنظُرْ هَلْ يُذْهِبَنَّ كَيْدُهُۥ مَا يَغِيظُ
Anaye dhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru (Mtume) katika dunia na Akhera na afunge kamba kwenye dari kisha aikate. Atazame je hila yake itaondoa hayo yaliyo mkasirisha?
وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَٰهُ ءَايَٰتٍۭ بَيِّنَٰتٍۢ وَأَنَّ ٱللَّهَ يَهْدِى مَن يُرِيدُ
Na namna hivi tumeiteremsha (Qur'ani) kuwa ni Aya zilizo wazi, na hakika Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye.
إِنَّ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَٱلَّذِينَ هَادُوا۟ وَٱلصَّٰبِـِٔينَ وَٱلنَّصَٰرَىٰ وَٱلْمَجُوسَ وَٱلَّذِينَ أَشْرَكُوٓا۟ إِنَّ ٱللَّهَ يَفْصِلُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ ٱلْقِيَٰمَةِ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ عَلَىٰ كُلِّ شَىْءٍۢ شَهِيدٌ
Hakika walio amini, na ambao ni Mayahudi na Wasabai na Wakristo na Majusi na wale walio shiriki - hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua baina yao Siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu.
أَلَمْ تَرَ أَنَّ ٱللَّهَ يَسْجُدُ لَهُۥ مَن فِى ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَمَن فِى ٱلْأَرْضِ وَٱلشَّمْسُ وَٱلْقَمَرُ وَٱلنُّجُومُ وَٱلْجِبَالُ وَٱلشَّجَرُ وَٱلدَّوَآبُّ وَكَثِيرٌۭ مِّنَ ٱلنَّاسِ ۖ وَكَثِيرٌ حَقَّ عَلَيْهِ ٱلْعَذَابُ ۗ وَمَن يُهِنِ ٱللَّهُ فَمَا لَهُۥ مِن مُّكْرِمٍ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ يَفْعَلُ مَا يَشَآءُ ۩
Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na anaye fedheheshwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo.
۞ هَٰذَانِ خَصْمَانِ ٱخْتَصَمُوا۟ فِى رَبِّهِمْ ۖ فَٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ قُطِّعَتْ لَهُمْ ثِيَابٌۭ مِّن نَّارٍۢ يُصَبُّ مِن فَوْقِ رُءُوسِهِمُ ٱلْحَمِيمُ
Hawa wagomvi wawili walio gombana kwa ajili ya Mola wao Mlezi. Basi walio kufuru watakatiwa nguo za moto, na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayo chemka.
يُصْهَرُ بِهِۦ مَا فِى بُطُونِهِمْ وَٱلْجُلُودُ
Kwa maji hayo vitayayushwa viliomo matumboni mwao, na ngozi zao pia.
وَلَهُم مَّقَٰمِعُ مِنْ حَدِيدٍۢ
Na kwa ajili yao yatakuwapo marungu ya chuma.
كُلَّمَآ أَرَادُوٓا۟ أَن يَخْرُجُوا۟ مِنْهَا مِنْ غَمٍّ أُعِيدُوا۟ فِيهَا وَذُوقُوا۟ عَذَابَ ٱلْحَرِيقِ
Kila wakitaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu watarudishwa humo humo, na wataambiwa: Onjeni adhabu ya kuungua!
إِنَّ ٱللَّهَ يُدْخِلُ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّٰلِحَٰتِ جَنَّٰتٍۢ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَٰرُ يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍۢ وَلُؤْلُؤًۭا ۖ وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌۭ
Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema katika Bustani zipitiwazo na mito kati yake. Watapambwa humo kwa mapambo ya mikononi ya dhahabu na lulu. Na mavazi yao humo ni hariri.
وَهُدُوٓا۟ إِلَى ٱلطَّيِّبِ مِنَ ٱلْقَوْلِ وَهُدُوٓا۟ إِلَىٰ صِرَٰطِ ٱلْحَمِيدِ
Na wataongozwa kwenye maneno mazuri, na wataongozwa kwenye Njia ya Msifiwa.
إِنَّ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ ٱللَّهِ وَٱلْمَسْجِدِ ٱلْحَرَامِ ٱلَّذِى جَعَلْنَٰهُ لِلنَّاسِ سَوَآءً ٱلْعَٰكِفُ فِيهِ وَٱلْبَادِ ۚ وَمَن يُرِدْ فِيهِ بِإِلْحَادٍۭ بِظُلْمٍۢ نُّذِقْهُ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍۢ
Hakika wale walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu na Msikiti Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakaye taka kufanya upotofu humo kwa dhulma, basi tutamwonjesha adhabu chungu.
وَإِذْ بَوَّأْنَا لِإِبْرَٰهِيمَ مَكَانَ ٱلْبَيْتِ أَن لَّا تُشْرِكْ بِى شَيْـًۭٔا وَطَهِّرْ بَيْتِىَ لِلطَّآئِفِينَ وَٱلْقَآئِمِينَ وَٱلرُّكَّعِ ٱلسُّجُودِ
Na pale tulipomweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba tukamwambia: Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya wanao izunguka kwa kut'ufu, na wanao kaa hapo kwa ibada, na wanao rukuu, na wanao sujudu.
وَأَذِّن فِى ٱلنَّاسِ بِٱلْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالًۭا وَعَلَىٰ كُلِّ ضَامِرٍۢ يَأْتِينَ مِن كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍۢ
Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.
لِّيَشْهَدُوا۟ مَنَٰفِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا۟ ٱسْمَ ٱللَّهِ فِىٓ أَيَّامٍۢ مَّعْلُومَٰتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّنۢ بَهِيمَةِ ٱلْأَنْعَٰمِ ۖ فَكُلُوا۟ مِنْهَا وَأَطْعِمُوا۟ ٱلْبَآئِسَ ٱلْفَقِيرَ
Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalumu juu ya nyama hoa alio waruzuku. Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri.
ثُمَّ لْيَقْضُوا۟ تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا۟ نُذُورَهُمْ وَلْيَطَّوَّفُوا۟ بِٱلْبَيْتِ ٱلْعَتِيقِ
Kisha wajisafishe taka zao, na waondoe nadhiri zao, na waizunguke Nyumba ya Kale.
ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ حُرُمَٰتِ ٱللَّهِ فَهُوَ خَيْرٌۭ لَّهُۥ عِندَ رَبِّهِۦ ۗ وَأُحِلَّتْ لَكُمُ ٱلْأَنْعَٰمُ إِلَّا مَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ ۖ فَٱجْتَنِبُوا۟ ٱلرِّجْسَ مِنَ ٱلْأَوْثَٰنِ وَٱجْتَنِبُوا۟ قَوْلَ ٱلزُّورِ
Ndio hivyo iwe! Na anaye vitukuza vitakatifu vya Mwenyezi Mungu basi hayo ndiyo kheri yake mbele ya Mola wake Mlezi. Na mmehalalishiwa nyama hoa ila wale mlio somewa. Basi jiepusheni na uchafu wa masanamu, na jiepusheni na usemi wa uwongo.
حُنَفَآءَ لِلَّهِ غَيْرَ مُشْرِكِينَ بِهِۦ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِٱللَّهِ فَكَأَنَّمَا خَرَّ مِنَ ٱلسَّمَآءِ فَتَخْطَفُهُ ٱلطَّيْرُ أَوْ تَهْوِى بِهِ ٱلرِّيحُ فِى مَكَانٍۢ سَحِيقٍۢ
Kwa kumtakasikia Imani Mwenyezi Mungu, bila ya kumshirikisha. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukamtupa pahala mbali.
ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَٰٓئِرَ ٱللَّهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى ٱلْقُلُوبِ
Ndio hivyo! Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo.
لَكُمْ فِيهَا مَنَٰفِعُ إِلَىٰٓ أَجَلٍۢ مُّسَمًّۭى ثُمَّ مَحِلُّهَآ إِلَى ٱلْبَيْتِ ٱلْعَتِيقِ
Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda maalumu. Kisha pahala pa kuchinjiwa kwake ni kwenye Nyumba ya Kale.
وَلِكُلِّ أُمَّةٍۢ جَعَلْنَا مَنسَكًۭا لِّيَذْكُرُوا۟ ٱسْمَ ٱللَّهِ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّنۢ بَهِيمَةِ ٱلْأَنْعَٰمِ ۗ فَإِلَٰهُكُمْ إِلَٰهٌۭ وَٰحِدٌۭ فَلَهُۥٓ أَسْلِمُوا۟ ۗ وَبَشِّرِ ٱلْمُخْبِتِينَ
Na kila umma tumewafanyia mahala pa kuchinjia mihanga ya ibada ili walitaje jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile walivyo ruzukiwa katika wanyama wa mifugo. Basi Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Jisalimishieni kwake tu, na wabashirie wanyenyekevu,
ٱلَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ ٱللَّهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَٱلصَّٰبِرِينَ عَلَىٰ مَآ أَصَابَهُمْ وَٱلْمُقِيمِى ٱلصَّلَوٰةِ وَمِمَّا رَزَقْنَٰهُمْ يُنفِقُونَ
Ambao, anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka, na wanao vumilia kwa yanao wasibu, na wanao shika Sala, na wanatoa katika tulivyo waruzuku.
وَٱلْبُدْنَ جَعَلْنَٰهَا لَكُم مِّن شَعَٰٓئِرِ ٱللَّهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌۭ ۖ فَٱذْكُرُوا۟ ٱسْمَ ٱللَّهِ عَلَيْهَا صَوَآفَّ ۖ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا۟ مِنْهَا وَأَطْعِمُوا۟ ٱلْقَانِعَ وَٱلْمُعْتَرَّ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرْنَٰهَا لَكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ
Na ngamia wa sadaka tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Mwenyezi Mungu; kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao wanapo simama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na walisheni walio kinai na wanao lazimika kuomba. Ndio kama hivi tumewafanya hawa wanyama dhalili kwenu ili mpate kushukuru.
لَن يَنَالَ ٱللَّهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَآؤُهَا وَلَٰكِن يَنَالُهُ ٱلتَّقْوَىٰ مِنكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا۟ ٱللَّهَ عَلَىٰ مَا هَدَىٰكُمْ ۗ وَبَشِّرِ ٱلْمُحْسِنِينَ
Nyama zao hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao, lakini unamfikia uchamngu wenu. Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyo kuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema.
۞ إِنَّ ٱللَّهَ يُدَٰفِعُ عَنِ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓا۟ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ خَوَّانٍۢ كَفُورٍ
Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walio amini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila khaini mwingi wa kukanya mema.
أُذِنَ لِلَّذِينَ يُقَٰتَلُونَ بِأَنَّهُمْ ظُلِمُوا۟ ۚ وَإِنَّ ٱللَّهَ عَلَىٰ نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ
Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia -
ٱلَّذِينَ أُخْرِجُوا۟ مِن دِيَٰرِهِم بِغَيْرِ حَقٍّ إِلَّآ أَن يَقُولُوا۟ رَبُّنَا ٱللَّهُ ۗ وَلَوْلَا دَفْعُ ٱللَّهِ ٱلنَّاسَ بَعْضَهُم بِبَعْضٍۢ لَّهُدِّمَتْ صَوَٰمِعُ وَبِيَعٌۭ وَصَلَوَٰتٌۭ وَمَسَٰجِدُ يُذْكَرُ فِيهَا ٱسْمُ ٱللَّهِ كَثِيرًۭا ۗ وَلَيَنصُرَنَّ ٱللَّهُ مَن يَنصُرُهُۥٓ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَقَوِىٌّ عَزِيزٌ
Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingeli vunjwa nymba za wat'awa, na makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu.
ٱلَّذِينَ إِن مَّكَّنَّٰهُمْ فِى ٱلْأَرْضِ أَقَامُوا۟ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتَوُا۟ ٱلزَّكَوٰةَ وَأَمَرُوا۟ بِٱلْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا۟ عَنِ ٱلْمُنكَرِ ۗ وَلِلَّهِ عَٰقِبَةُ ٱلْأُمُورِ
Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Sala, na wakatoa Zaka, na wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote.
وَإِن يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍۢ وَعَادٌۭ وَثَمُودُ
Na wakikukanusha basi walikwisha kanusha kabla yao watu wa Nuhu, na kina A'ad na kina Thamud,
وَقَوْمُ إِبْرَٰهِيمَ وَقَوْمُ لُوطٍۢ
Na watu wa Ibrahim na watu wa Lut'i
وَأَصْحَٰبُ مَدْيَنَ ۖ وَكُذِّبَ مُوسَىٰ فَأَمْلَيْتُ لِلْكَٰفِرِينَ ثُمَّ أَخَذْتُهُمْ ۖ فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ
Na watu wa Madiana. Na Musa pia alikanushwa. Nikawapa muda makafiri, kisha nikawatia mkononi. Basi ilikuwaje adhabu yangu!
فَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَٰهَا وَهِىَ ظَالِمَةٌۭ فَهِىَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا وَبِئْرٍۢ مُّعَطَّلَةٍۢ وَقَصْرٍۢ مَّشِيدٍ
Miji mingapi tuliiangamiza iliyo kuwa ikidhulumu, ikawa imebaki magofu, na visima vilivyo achwa, na majumba yaliyo kuwa madhubuti?
أَفَلَمْ يَسِيرُوا۟ فِى ٱلْأَرْضِ فَتَكُونَ لَهُمْ قُلُوبٌۭ يَعْقِلُونَ بِهَآ أَوْ ءَاذَانٌۭ يَسْمَعُونَ بِهَا ۖ فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى ٱلْأَبْصَٰرُ وَلَٰكِن تَعْمَى ٱلْقُلُوبُ ٱلَّتِى فِى ٱلصُّدُورِ
Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo zao za kuzingatia, au masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayo pofuka, lakini zinazo pofuka ni nyoyo ziliomo vifuani.
وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِٱلْعَذَابِ وَلَن يُخْلِفَ ٱللَّهُ وَعْدَهُۥ ۚ وَإِنَّ يَوْمًا عِندَ رَبِّكَ كَأَلْفِ سَنَةٍۢ مِّمَّا تَعُدُّونَ
Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini Mwenyezi Mungu hatakwenda kinyume na ahadi yake kabisa. Na hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi.
وَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ أَمْلَيْتُ لَهَا وَهِىَ ظَالِمَةٌۭ ثُمَّ أَخَذْتُهَا وَإِلَىَّ ٱلْمَصِيرُ
Na miji mingapi niliipa muda na hali ilikuwa imedhulumu, na kisha nikaitia mkononi? Na kwangu Mimi ndio marudio yote.
قُلْ يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ إِنَّمَآ أَنَا۠ لَكُمْ نَذِيرٌۭ مُّبِينٌۭ
Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni mwonyaji kwenu niliye dhaahiri.
فَٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّٰلِحَٰتِ لَهُم مَّغْفِرَةٌۭ وَرِزْقٌۭ كَرِيمٌۭ
Basi walio amini na wakatenda mema watapata maghfira na riziki za ukarimu.
وَٱلَّذِينَ سَعَوْا۟ فِىٓ ءَايَٰتِنَا مُعَٰجِزِينَ أُو۟لَٰٓئِكَ أَصْحَٰبُ ٱلْجَحِيمِ
Na wanao jitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa Motoni.
وَمَآ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍۢ وَلَا نَبِىٍّ إِلَّآ إِذَا تَمَنَّىٰٓ أَلْقَى ٱلشَّيْطَٰنُ فِىٓ أُمْنِيَّتِهِۦ فَيَنسَخُ ٱللَّهُ مَا يُلْقِى ٱلشَّيْطَٰنُ ثُمَّ يُحْكِمُ ٱللَّهُ ءَايَٰتِهِۦ ۗ وَٱللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌۭ
Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii ila anapo soma, Shet'ani hutumbukiza katika masomo yake. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayo yatia Shet'ani; kisha Mwenyezi Mungu huzithibitisha Aya zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
لِّيَجْعَلَ مَا يُلْقِى ٱلشَّيْطَٰنُ فِتْنَةًۭ لِّلَّذِينَ فِى قُلُوبِهِم مَّرَضٌۭ وَٱلْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُمْ ۗ وَإِنَّ ٱلظَّٰلِمِينَ لَفِى شِقَاقٍۭ بَعِيدٍۢ
Hayo ni ili alifanye lile analo litia Shet'ani liwe ni fitna kwa wale wenye maradhi ndani ya nyoyo zao, na wale ambao nyoyo zao ni ngumu. Na hakika madhaalimu wamo katika mfarakano wa mbali.
وَلِيَعْلَمَ ٱلَّذِينَ أُوتُوا۟ ٱلْعِلْمَ أَنَّهُ ٱلْحَقُّ مِن رَّبِّكَ فَيُؤْمِنُوا۟ بِهِۦ فَتُخْبِتَ لَهُۥ قُلُوبُهُمْ ۗ وَإِنَّ ٱللَّهَ لَهَادِ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓا۟ إِلَىٰ صِرَٰطٍۢ مُّسْتَقِيمٍۢ
Na ili walio pewa ilimu wajue kuwa hayo ni Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi na waamini, na zipate kutua nyoyo zao. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye anaye waongoa wenye kuamini kwenye Njia Iliyo Nyooka.
وَلَا يَزَالُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ فِى مِرْيَةٍۢ مِّنْهُ حَتَّىٰ تَأْتِيَهُمُ ٱلسَّاعَةُ بَغْتَةً أَوْ يَأْتِيَهُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَقِيمٍ
Na walio kufuru hawatoacha kuwa katika wasiwasi kwa hilo mpaka Saa iwafikie ghafla, au iwafikie adhabu ya Siku Tasa.
ٱلْمُلْكُ يَوْمَئِذٍۢ لِّلَّهِ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ ۚ فَٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّٰلِحَٰتِ فِى جَنَّٰتِ ٱلنَّعِيمِ
Ufalme wote siku hiyo utakuwa wa Mwenyezi Mungu. Atahukumu baina yao. Basi walio amini na wakatenda mema watakuwa katika Bustani zenye neema.
وَٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ وَكَذَّبُوا۟ بِـَٔايَٰتِنَا فَأُو۟لَٰٓئِكَ لَهُمْ عَذَابٌۭ مُّهِينٌۭ
Na walio kufuru na kuzikanusha Ishara zetu, basi hao watapata adhabu ya kufedhehesha.
وَٱلَّذِينَ هَاجَرُوا۟ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ ثُمَّ قُتِلُوٓا۟ أَوْ مَاتُوا۟ لَيَرْزُقَنَّهُمُ ٱللَّهُ رِزْقًا حَسَنًۭا ۚ وَإِنَّ ٱللَّهَ لَهُوَ خَيْرُ ٱلرَّٰزِقِينَ
Na walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kisha wakauwawa au wakafa, bila ya shaka Mwenyezi Mungu atawaruzuku riziki njema. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mbora wa wanao ruzuku.
لَيُدْخِلَنَّهُم مُّدْخَلًۭا يَرْضَوْنَهُۥ ۗ وَإِنَّ ٱللَّهَ لَعَلِيمٌ حَلِيمٌۭ
BIla ya shaka atawaingiza pahala watakapo paridhia. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole.
۞ ذَٰلِكَ وَمَنْ عَاقَبَ بِمِثْلِ مَا عُوقِبَ بِهِۦ ثُمَّ بُغِىَ عَلَيْهِ لَيَنصُرَنَّهُ ٱللَّهُ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَعَفُوٌّ غَفُورٌۭ
Ndio namna hivi. Na anaye lipiza mfano wa alivyo adhibiwa, kisha akadhulumiwa, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atamsaidia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye maghfira.
ذَٰلِكَ بِأَنَّ ٱللَّهَ يُولِجُ ٱلَّيْلَ فِى ٱلنَّهَارِ وَيُولِجُ ٱلنَّهَارَ فِى ٱلَّيْلِ وَأَنَّ ٱللَّهَ سَمِيعٌۢ بَصِيرٌۭ
Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu huingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
ذَٰلِكَ بِأَنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِۦ هُوَ ٱلْبَٰطِلُ وَأَنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلْعَلِىُّ ٱلْكَبِيرُ
Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Wa Kweli, na kwamba wale wanao waomba badala yake, ni baat'ili, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliye Juu na ndiye Mkubwa.
أَلَمْ تَرَ أَنَّ ٱللَّهَ أَنزَلَ مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءًۭ فَتُصْبِحُ ٱلْأَرْضُ مُخْضَرَّةً ۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌۭ
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu huteremsha maji kutoka mbinguni, na mara ardhi inakuwa chanikiwiti? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole na Mwenye kujua.
لَّهُۥ مَا فِى ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَمَا فِى ٱلْأَرْضِ ۗ وَإِنَّ ٱللَّهَ لَهُوَ ٱلْغَنِىُّ ٱلْحَمِيدُ
Ni vyake viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Mwenye kusifiwa.
أَلَمْ تَرَ أَنَّ ٱللَّهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِى ٱلْأَرْضِ وَٱلْفُلْكَ تَجْرِى فِى ٱلْبَحْرِ بِأَمْرِهِۦ وَيُمْسِكُ ٱلسَّمَآءَ أَن تَقَعَ عَلَى ٱلْأَرْضِ إِلَّا بِإِذْنِهِۦٓ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ بِٱلنَّاسِ لَرَءُوفٌۭ رَّحِيمٌۭ
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu.
وَهُوَ ٱلَّذِىٓ أَحْيَاكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ۗ إِنَّ ٱلْإِنسَٰنَ لَكَفُورٌۭ
Na Yeye ndiye aliye kuhuisheni kisha akakufisheni, na kisha atakufufueni. Hakika mwanaadamu hana fadhila.
لِّكُلِّ أُمَّةٍۢ جَعَلْنَا مَنسَكًا هُمْ نَاسِكُوهُ ۖ فَلَا يُنَٰزِعُنَّكَ فِى ٱلْأَمْرِ ۚ وَٱدْعُ إِلَىٰ رَبِّكَ ۖ إِنَّكَ لَعَلَىٰ هُدًۭى مُّسْتَقِيمٍۢ
Kila umma tumewajaalia na ibada zao wanazo zishika. Basi wasizozane nawe katika jambo hili. Na waite watu kwendea kwa Mola wako Mlezi. Hakika wewe uko kwenye Uwongofu Ulio Nyooka.
وَإِن جَٰدَلُوكَ فَقُلِ ٱللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا تَعْمَلُونَ
Na wakikujadili basi sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi mnayo yatenda.
ٱللَّهُ يَحْكُمُ بَيْنَكُمْ يَوْمَ ٱلْقِيَٰمَةِ فِيمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ
Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu Siku ya Kiyama katika hayo mnayo khitalifiana.
أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ ٱللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِى ٱلسَّمَآءِ وَٱلْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِى كِتَٰبٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى ٱللَّهِ يَسِيرٌۭ
Je! Hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ ٱللَّهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِۦ سُلْطَٰنًۭا وَمَا لَيْسَ لَهُم بِهِۦ عِلْمٌۭ ۗ وَمَا لِلظَّٰلِمِينَ مِن نَّصِيرٍۢ
Na wanaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ambavyo hakuviteremshia ushahidi, na ambavyo hawana ujuzi navyo. Na madhaalimu hawatakuwa na wa kuwasaidia.
وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ ءَايَٰتُنَا بَيِّنَٰتٍۢ تَعْرِفُ فِى وُجُوهِ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ ٱلْمُنكَرَ ۖ يَكَادُونَ يَسْطُونَ بِٱلَّذِينَ يَتْلُونَ عَلَيْهِمْ ءَايَٰتِنَا ۗ قُلْ أَفَأُنَبِّئُكُم بِشَرٍّۢ مِّن ذَٰلِكُمُ ۗ ٱلنَّارُ وَعَدَهَا ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ ۖ وَبِئْسَ ٱلْمَصِيرُ
Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi utaona chuki katika nyuso za walio kufuru. Hukaribia kuwavamia wale wanao wasomea hizo Aya zetu. Sema: Je! Nikwambieni yaliyo mabaya zaidi kuliko haya? Ni Moto. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio kufuru, na ni marudio mabaya hayo.
يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ ضُرِبَ مَثَلٌۭ فَٱسْتَمِعُوا۟ لَهُۥٓ ۚ إِنَّ ٱلَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ ٱللَّهِ لَن يَخْلُقُوا۟ ذُبَابًۭا وَلَوِ ٱجْتَمَعُوا۟ لَهُۥ ۖ وَإِن يَسْلُبْهُمُ ٱلذُّبَابُ شَيْـًۭٔا لَّا يَسْتَنقِذُوهُ مِنْهُ ۚ ضَعُفَ ٱلطَّالِبُ وَٱلْمَطْلُوبُ
Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoumba hata nzi ijapo kuwa watajumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika kweli huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa.
مَا قَدَرُوا۟ ٱللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِۦٓ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَقَوِىٌّ عَزِيزٌ
Hawakumuadhimisha Mwenyezi Mungu anavyo stahiki kuadhimishwa. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye kushinda.
ٱللَّهُ يَصْطَفِى مِنَ ٱلْمَلَٰٓئِكَةِ رُسُلًۭا وَمِنَ ٱلنَّاسِ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ سَمِيعٌۢ بَصِيرٌۭ
Mwenyezi Mungu huteuwa Wajumbe miongoni mwa Malaika na miongoni mwa watu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۗ وَإِلَى ٱللَّهِ تُرْجَعُ ٱلْأُمُورُ
Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Na kwa Mwenyezi Mungu yatarejeshwa mambo yote.
يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ ٱرْكَعُوا۟ وَٱسْجُدُوا۟ وَٱعْبُدُوا۟ رَبَّكُمْ وَٱفْعَلُوا۟ ٱلْخَيْرَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ۩
Enyi mlio amini! Rukuuni na msujudu, na muabuduni Mola wenu Mlezi, na tendeni mema, ili mfanikiwe.
وَجَٰهِدُوا۟ فِى ٱللَّهِ حَقَّ جِهَادِهِۦ ۚ هُوَ ٱجْتَبَىٰكُمْ وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِى ٱلدِّينِ مِنْ حَرَجٍۢ ۚ مِّلَّةَ أَبِيكُمْ إِبْرَٰهِيمَ ۚ هُوَ سَمَّىٰكُمُ ٱلْمُسْلِمِينَ مِن قَبْلُ وَفِى هَٰذَا لِيَكُونَ ٱلرَّسُولُ شَهِيدًا عَلَيْكُمْ وَتَكُونُوا۟ شُهَدَآءَ عَلَى ٱلنَّاسِ ۚ فَأَقِيمُوا۟ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتُوا۟ ٱلزَّكَوٰةَ وَٱعْتَصِمُوا۟ بِٱللَّهِ هُوَ مَوْلَىٰكُمْ ۖ فَنِعْمَ ٱلْمَوْلَىٰ وَنِعْمَ ٱلنَّصِيرُ
Na fanyeni juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama inavyo stahiki jihadi yake. Yeye amekuteueni. Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim. Yeye (Mwenyezi Mungu) alikuiteni Waislamu tangu zamani, na katika hii (Qur'ani) pia, ili awe Mtume shahidi juu yenu, na nyinyi muwe mashahidi kwa watu. Basi shikeni Sala na toeni Zaka na shikamaneni na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mlinzi wenu, Mlinzi bora kabisa, na Msaidizi bora kabisa.