Surah 12: Yusuf — يوسف

۞ وَمَآ أُبَرِّئُ نَفْسِىٓ ۚ إِنَّ ٱلنَّفْسَ لَأَمَّارَةٌۢ بِٱلسُّوٓءِ إِلَّا مَا رَحِمَ رَبِّىٓ ۚ إِنَّ رَبِّى غَفُورٌۭ رَّحِيمٌۭ
NAMI sijitoi lawamani. Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu, isipo kuwa ile ambayo Mola wangu Mlezi aliyo irehemu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.
وَقَالَ ٱلْمَلِكُ ٱئْتُونِى بِهِۦٓ أَسْتَخْلِصْهُ لِنَفْسِى ۖ فَلَمَّا كَلَّمَهُۥ قَالَ إِنَّكَ ٱلْيَوْمَ لَدَيْنَا مَكِينٌ أَمِينٌۭ
Basi mfalme akasema: Mleteni kwangu, awe wangu mwenyewe khasa. Basi alipo msemeza alinena: Hakika wewe leo umekwisha tamakani kwetu na umeaminika.
قَالَ ٱجْعَلْنِى عَلَىٰ خَزَآئِنِ ٱلْأَرْضِ ۖ إِنِّى حَفِيظٌ عَلِيمٌۭ
Yusuf akasema: Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani hakika mimi ni mlinzi mjuzi.
وَكَذَٰلِكَ مَكَّنَّا لِيُوسُفَ فِى ٱلْأَرْضِ يَتَبَوَّأُ مِنْهَا حَيْثُ يَشَآءُ ۚ نُصِيبُ بِرَحْمَتِنَا مَن نَّشَآءُ ۖ وَلَا نُضِيعُ أَجْرَ ٱلْمُحْسِنِينَ
Basi namna hivi tukampa Yusuf cheo katika nchi; anakaa humo popote anapo penda. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupuuzi malipo ya wafanyao mema.
وَلَأَجْرُ ٱلْءَاخِرَةِ خَيْرٌۭ لِّلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَكَانُوا۟ يَتَّقُونَ
Na hakika malipo ya Akhera ni bora zaidi, kwa walio amini na wakawa wachamngu.
وَجَآءَ إِخْوَةُ يُوسُفَ فَدَخَلُوا۟ عَلَيْهِ فَعَرَفَهُمْ وَهُمْ لَهُۥ مُنكِرُونَ
Wakaja ndugu zake Yusuf, na wakaingia kwake. Yeye akawajua na wao hawakumjua.
وَلَمَّا جَهَّزَهُم بِجَهَازِهِمْ قَالَ ٱئْتُونِى بِأَخٍۢ لَّكُم مِّنْ أَبِيكُمْ ۚ أَلَا تَرَوْنَ أَنِّىٓ أُوفِى ٱلْكَيْلَ وَأَنَا۠ خَيْرُ ٱلْمُنزِلِينَ
Na alipo watengenezea tayari haja yao alisema: Nileteeni ndugu yenu kwa baba. Je! Hamwoni ya kwamba mimi ninatimiza kipimo, nami ni mbora wa kukirimu?
فَإِن لَّمْ تَأْتُونِى بِهِۦ فَلَا كَيْلَ لَكُمْ عِندِى وَلَا تَقْرَبُونِ
Na msipo niletea basi hampati kipimo chochote kwangu, wala msinikurubie.
قَالُوا۟ سَنُرَٰوِدُ عَنْهُ أَبَاهُ وَإِنَّا لَفَٰعِلُونَ
Wakasema: Sisi tutamrairai baba yake; na bila ya shaka tutafanya hayo.
وَقَالَ لِفِتْيَٰنِهِ ٱجْعَلُوا۟ بِضَٰعَتَهُمْ فِى رِحَالِهِمْ لَعَلَّهُمْ يَعْرِفُونَهَآ إِذَا ٱنقَلَبُوٓا۟ إِلَىٰٓ أَهْلِهِمْ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ
Na Yusuf akawaambia watumishi wake: Tieni bidhaa zao katika mizigo yao, ili wazione watakapo rudi kwa watu wao wapate kurejea tena.
فَلَمَّا رَجَعُوٓا۟ إِلَىٰٓ أَبِيهِمْ قَالُوا۟ يَٰٓأَبَانَا مُنِعَ مِنَّا ٱلْكَيْلُ فَأَرْسِلْ مَعَنَآ أَخَانَا نَكْتَلْ وَإِنَّا لَهُۥ لَحَٰفِظُونَ
Basi walipo rejea kwa baba yao, walisema: Ewe baba yetu! Tumenyimwa chakula zaidi, basi mpeleke nasi ndugu yetu ili tupate kupimiwa; na yakini sisi tutamlinda.
قَالَ هَلْ ءَامَنُكُمْ عَلَيْهِ إِلَّا كَمَآ أَمِنتُكُمْ عَلَىٰٓ أَخِيهِ مِن قَبْلُ ۖ فَٱللَّهُ خَيْرٌ حَٰفِظًۭا ۖ وَهُوَ أَرْحَمُ ٱلرَّٰحِمِينَ
Je, nikuaminini kwa huyu ila kama nilivyo kuaminini kwa nduguye zamani? Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kulinda, naye ndiye Mbora wa kurehemu kuliko wenye kurehemu wote.
وَلَمَّا فَتَحُوا۟ مَتَٰعَهُمْ وَجَدُوا۟ بِضَٰعَتَهُمْ رُدَّتْ إِلَيْهِمْ ۖ قَالُوا۟ يَٰٓأَبَانَا مَا نَبْغِى ۖ هَٰذِهِۦ بِضَٰعَتُنَا رُدَّتْ إِلَيْنَا ۖ وَنَمِيرُ أَهْلَنَا وَنَحْفَظُ أَخَانَا وَنَزْدَادُ كَيْلَ بَعِيرٍۢ ۖ ذَٰلِكَ كَيْلٌۭ يَسِيرٌۭ
Na walipo fungua mizigo yao wakakuta bidhaa zao wamerudishiwa. Wakasema: Ewe baba yetu! Tutake nini zaidi? Hizi bidhaa zetu tumerudishiwa. Wacha tuwaletee watu wetu chakula, na tutamlinda ndugu yetu, na tutaongeza shehena ya ngamia. Na hicho ni kipimo kidogo.
قَالَ لَنْ أُرْسِلَهُۥ مَعَكُمْ حَتَّىٰ تُؤْتُونِ مَوْثِقًۭا مِّنَ ٱللَّهِ لَتَأْتُنَّنِى بِهِۦٓ إِلَّآ أَن يُحَاطَ بِكُمْ ۖ فَلَمَّآ ءَاتَوْهُ مَوْثِقَهُمْ قَالَ ٱللَّهُ عَلَىٰ مَا نَقُولُ وَكِيلٌۭ
Akasema: Sitampeleka nanyi mpaka mnipe ahadi kwa Mwenyezi Mungu kwamba lazima mtamrejeza kwangu, ila ikiwa mmezungukwa. Basi walipo mpa ahadi yao alisema: Mwenyezi Mungu ndiye Mtegemewa kwa tuyasemayo.
وَقَالَ يَٰبَنِىَّ لَا تَدْخُلُوا۟ مِنۢ بَابٍۢ وَٰحِدٍۢ وَٱدْخُلُوا۟ مِنْ أَبْوَٰبٍۢ مُّتَفَرِّقَةٍۢ ۖ وَمَآ أُغْنِى عَنكُم مِّنَ ٱللَّهِ مِن شَىْءٍ ۖ إِنِ ٱلْحُكْمُ إِلَّا لِلَّهِ ۖ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ ۖ وَعَلَيْهِ فَلْيَتَوَكَّلِ ٱلْمُتَوَكِّلُونَ
Na akasema: Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja, bali ingieni kwa milango mbali mbali. Wala mimi sikufaeni kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Hukumu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu tu. Juu yake Yeye mimi nimetegemea, na juu yake Yeye wategemee wanao tegemea.
وَلَمَّا دَخَلُوا۟ مِنْ حَيْثُ أَمَرَهُمْ أَبُوهُم مَّا كَانَ يُغْنِى عَنْهُم مِّنَ ٱللَّهِ مِن شَىْءٍ إِلَّا حَاجَةًۭ فِى نَفْسِ يَعْقُوبَ قَضَىٰهَا ۚ وَإِنَّهُۥ لَذُو عِلْمٍۢ لِّمَا عَلَّمْنَٰهُ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ ٱلنَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ
Na walipo ingia kama alivyo waamrisha baba yao, haikuwafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu, isipo kuwa ni haja tu iliyo kuwa katika nafsi ya Yaa'qub aliitimiza. Na hakika yeye alikuwa na ilimu kwa sababu tulimfundisha; lakini watu wengi hawajui.
وَلَمَّا دَخَلُوا۟ عَلَىٰ يُوسُفَ ءَاوَىٰٓ إِلَيْهِ أَخَاهُ ۖ قَالَ إِنِّىٓ أَنَا۠ أَخُوكَ فَلَا تَبْتَئِسْ بِمَا كَانُوا۟ يَعْمَلُونَ
Na walipo ingia kwa Yusuf alimchukua nduguye akasema: Mimi hakika ni nduguyo. Basi usihuzunike kwa waliyo kuwa wakiyafanya.
فَلَمَّا جَهَّزَهُم بِجَهَازِهِمْ جَعَلَ ٱلسِّقَايَةَ فِى رَحْلِ أَخِيهِ ثُمَّ أَذَّنَ مُؤَذِّنٌ أَيَّتُهَا ٱلْعِيرُ إِنَّكُمْ لَسَٰرِقُونَ
Na alipo kwisha watengenezea mahitaji yao akakitia kikopo cha kunywea maji katika mzigo wa nduguye huyo, kisha mnadi akanadi: Enyi wasafiri! Hapana shaka nyinyi ni wezi!
قَالُوا۟ وَأَقْبَلُوا۟ عَلَيْهِم مَّاذَا تَفْقِدُونَ
Wakasema nao wamewakabili: Kwani mmepoteza nini?
قَالُوا۟ نَفْقِدُ صُوَاعَ ٱلْمَلِكِ وَلِمَن جَآءَ بِهِۦ حِمْلُ بَعِيرٍۢ وَأَنَا۠ بِهِۦ زَعِيمٌۭ
Wakasema: Tumepoteza kopo la mfalme. Na ataye lileta atapewa shehena nzima ya ngamia. Nami ni dhaamini wa hayo.
قَالُوا۟ تَٱللَّهِ لَقَدْ عَلِمْتُم مَّا جِئْنَا لِنُفْسِدَ فِى ٱلْأَرْضِ وَمَا كُنَّا سَٰرِقِينَ
Wakasema: Wallahi! Mnajua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya uharibifu katika nchi hii, wala sisi si wezi.
قَالُوا۟ فَمَا جَزَٰٓؤُهُۥٓ إِن كُنتُمْ كَٰذِبِينَ
Wakasema: Basi malipo yake yatakuwa nini ikiwa nyinyi ni waongo?
قَالُوا۟ جَزَٰٓؤُهُۥ مَن وُجِدَ فِى رَحْلِهِۦ فَهُوَ جَزَٰٓؤُهُۥ ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِى ٱلظَّٰلِمِينَ
Wakasema: Malipo yake ni yule ambaye ataonekana nalo yeye huyo ndiye malipo yake. Hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu.
فَبَدَأَ بِأَوْعِيَتِهِمْ قَبْلَ وِعَآءِ أَخِيهِ ثُمَّ ٱسْتَخْرَجَهَا مِن وِعَآءِ أَخِيهِ ۚ كَذَٰلِكَ كِدْنَا لِيُوسُفَ ۖ مَا كَانَ لِيَأْخُذَ أَخَاهُ فِى دِينِ ٱلْمَلِكِ إِلَّآ أَن يَشَآءَ ٱللَّهُ ۚ نَرْفَعُ دَرَجَٰتٍۢ مَّن نَّشَآءُ ۗ وَفَوْقَ كُلِّ ذِى عِلْمٍ عَلِيمٌۭ
Basi akaanza kwenye mizigo yao kabla ya mzigo wa nduguye. Kisha akakitoa katika mzigo wa nduguye. Hivi ndivyo tulivyo mpangia Yusuf. Hakuweza kumzuia nduguye kwa sharia ya mfalme isipo kuwa alivyo taka Mwenyezi Mungu. Tunawatukuza kwenye vyeo tuwatakao; na juu ya kila ajuaye yupo ajuaye zaidi.
۞ قَالُوٓا۟ إِن يَسْرِقْ فَقَدْ سَرَقَ أَخٌۭ لَّهُۥ مِن قَبْلُ ۚ فَأَسَرَّهَا يُوسُفُ فِى نَفْسِهِۦ وَلَمْ يُبْدِهَا لَهُمْ ۚ قَالَ أَنتُمْ شَرٌّۭ مَّكَانًۭا ۖ وَٱللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا تَصِفُونَ
Wakasema: Ikiwa huyu ameiba, basi nduguye vile vile aliiba zamani. Lakini Yusuf aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwaonyesha. Akawaambia: Nyinyi mko katika hali mbaya zaidi, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi hayo mnayo singizia.
قَالُوا۟ يَٰٓأَيُّهَا ٱلْعَزِيزُ إِنَّ لَهُۥٓ أَبًۭا شَيْخًۭا كَبِيرًۭا فَخُذْ أَحَدَنَا مَكَانَهُۥٓ ۖ إِنَّا نَرَىٰكَ مِنَ ٱلْمُحْسِنِينَ
Wakasema: Ewe Mheshimiwa! Huyu anaye baba mzee sana. Kwa hivyo mchukue mmoja wetu badala yake. Hakika sisi tunakuona wewe ni katika watu wema.
قَالَ مَعَاذَ ٱللَّهِ أَن نَّأْخُذَ إِلَّا مَن وَجَدْنَا مَتَٰعَنَا عِندَهُۥٓ إِنَّآ إِذًۭا لَّظَٰلِمُونَ
Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali kumshika yeyote yule isipo kuwa tuliye mkuta naye kitu chetu. Hivyo basi tutakuwa wenye kudhulumu.
فَلَمَّا ٱسْتَيْـَٔسُوا۟ مِنْهُ خَلَصُوا۟ نَجِيًّۭا ۖ قَالَ كَبِيرُهُمْ أَلَمْ تَعْلَمُوٓا۟ أَنَّ أَبَاكُمْ قَدْ أَخَذَ عَلَيْكُم مَّوْثِقًۭا مِّنَ ٱللَّهِ وَمِن قَبْلُ مَا فَرَّطتُمْ فِى يُوسُفَ ۖ فَلَنْ أَبْرَحَ ٱلْأَرْضَ حَتَّىٰ يَأْذَنَ لِىٓ أَبِىٓ أَوْ يَحْكُمَ ٱللَّهُ لِى ۖ وَهُوَ خَيْرُ ٱلْحَٰكِمِينَ
Walipo kata tamaa naye wakenda kando kunong'ona. Mkubwa wao akasema: Je! Hamjui ya kwamba baba yenu amechukua ahadi kwenu kutokana na Mwenyezi Mungu, na kabla ya hapo mlimkosa katika agano lenu juu ya Yusuf? Basi mimi sitotoka nchi hii mpaka baba yangu anipe ruhusa au Mwenyezi Mungu anihukumie. Na Yeye ndiye Mbora wa mahakimu.
ٱرْجِعُوٓا۟ إِلَىٰٓ أَبِيكُمْ فَقُولُوا۟ يَٰٓأَبَانَآ إِنَّ ٱبْنَكَ سَرَقَ وَمَا شَهِدْنَآ إِلَّا بِمَا عَلِمْنَا وَمَا كُنَّا لِلْغَيْبِ حَٰفِظِينَ
Rudini kwa baba yenu, na mwambieni: Ee baba yetu! Mwanao ameiba. Na sisi hatutoi ushahidi ila kwa tunayo yajua. Wala sisi hatukuwa wenye kuhifadhi mambo ya ghaibu.
وَسْـَٔلِ ٱلْقَرْيَةَ ٱلَّتِى كُنَّا فِيهَا وَٱلْعِيرَ ٱلَّتِىٓ أَقْبَلْنَا فِيهَا ۖ وَإِنَّا لَصَٰدِقُونَ
Na waulize watu wa mji tulio kuwako, na msafara tulio kuja nao. Na hakika sisi tunasema kweli.
قَالَ بَلْ سَوَّلَتْ لَكُمْ أَنفُسُكُمْ أَمْرًۭا ۖ فَصَبْرٌۭ جَمِيلٌ ۖ عَسَى ٱللَّهُ أَن يَأْتِيَنِى بِهِمْ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُۥ هُوَ ٱلْعَلِيمُ ٱلْحَكِيمُ
Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kwenye jambo fulani. Subira ni njema! Asaa Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima.
وَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَٰٓأَسَفَىٰ عَلَىٰ يُوسُفَ وَٱبْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ ٱلْحُزْنِ فَهُوَ كَظِيمٌۭ
Naye akajitenga nao, na akasema: Ah! Masikini Yusuf! Na macho yake yakawa meupe kwa huzuni aliyo kuwa akiizuia.
قَالُوا۟ تَٱللَّهِ تَفْتَؤُا۟ تَذْكُرُ يُوسُفَ حَتَّىٰ تَكُونَ حَرَضًا أَوْ تَكُونَ مِنَ ٱلْهَٰلِكِينَ
Wakasema: Wallahi! Huachi kumkumbuka Yusuf mpaka uwe mgonjwa au uwe katika walio hiliki.
قَالَ إِنَّمَآ أَشْكُوا۟ بَثِّى وَحُزْنِىٓ إِلَى ٱللَّهِ وَأَعْلَمُ مِنَ ٱللَّهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ
Akasema: Hakika mimi namshitakia Mwenyezi Mungu sikitiko langu na huzuni yangu. Na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi.
يَٰبَنِىَّ ٱذْهَبُوا۟ فَتَحَسَّسُوا۟ مِن يُوسُفَ وَأَخِيهِ وَلَا تَا۟يْـَٔسُوا۟ مِن رَّوْحِ ٱللَّهِ ۖ إِنَّهُۥ لَا يَا۟يْـَٔسُ مِن رَّوْحِ ٱللَّهِ إِلَّا ٱلْقَوْمُ ٱلْكَٰفِرُونَ
Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye, wala msikate tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu isipo kuwa watu makafiri.
فَلَمَّا دَخَلُوا۟ عَلَيْهِ قَالُوا۟ يَٰٓأَيُّهَا ٱلْعَزِيزُ مَسَّنَا وَأَهْلَنَا ٱلضُّرُّ وَجِئْنَا بِبِضَٰعَةٍۢ مُّزْجَىٰةٍۢ فَأَوْفِ لَنَا ٱلْكَيْلَ وَتَصَدَّقْ عَلَيْنَآ ۖ إِنَّ ٱللَّهَ يَجْزِى ٱلْمُتَصَدِّقِينَ
Basi walipo ingia kwa Yusuf walisema: Ewe Mheshimiwa! Imetupata shida, sisi na watu wetu. Na tumeleta mali kidogo. Basi tupimie kipimo na fanya kama unatupa sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa watoao sadaka.
قَالَ هَلْ عَلِمْتُم مَّا فَعَلْتُم بِيُوسُفَ وَأَخِيهِ إِذْ أَنتُمْ جَٰهِلُونَ
Akasema: Je! Mmejua mliyo mfanyia Yusuf na nduguye mlipo kuwa wajinga?
قَالُوٓا۟ أَءِنَّكَ لَأَنتَ يُوسُفُ ۖ قَالَ أَنَا۠ يُوسُفُ وَهَٰذَآ أَخِى ۖ قَدْ مَنَّ ٱللَّهُ عَلَيْنَآ ۖ إِنَّهُۥ مَن يَتَّقِ وَيَصْبِرْ فَإِنَّ ٱللَّهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ ٱلْمُحْسِنِينَ
Wakasema: Kumbe wewe ndiye Yusuf? Akasema: Mimi ndiye Yusuf, na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu ametufanyia hisani. Hakika anaye mcha Mungu na akasubiri, basi Mwenyezi Mungu haachi ukapotea ujira wa wafanyao mema.
قَالُوا۟ تَٱللَّهِ لَقَدْ ءَاثَرَكَ ٱللَّهُ عَلَيْنَا وَإِن كُنَّا لَخَٰطِـِٔينَ
Wakasema: Wallahi! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha wewe kuliko sisi, na hakika sisi tulikuwa wenye kukosa.
قَالَ لَا تَثْرِيبَ عَلَيْكُمُ ٱلْيَوْمَ ۖ يَغْفِرُ ٱللَّهُ لَكُمْ ۖ وَهُوَ أَرْحَمُ ٱلرَّٰحِمِينَ
Akasema: Leo hapana lawama juu yenu. Mwenyezi Mungu atakusameheni, naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanao rehemu.
ٱذْهَبُوا۟ بِقَمِيصِى هَٰذَا فَأَلْقُوهُ عَلَىٰ وَجْهِ أَبِى يَأْتِ بَصِيرًۭا وَأْتُونِى بِأَهْلِكُمْ أَجْمَعِينَ
Nendeni na kanzu yangu hii na mumwekee usoni baba yangu, atakuwa mwenye kuona. Na mje nao watu wenu wote wa nyumbani.
وَلَمَّا فَصَلَتِ ٱلْعِيرُ قَالَ أَبُوهُمْ إِنِّى لَأَجِدُ رِيحَ يُوسُفَ ۖ لَوْلَآ أَن تُفَنِّدُونِ
Na ulipo ondoka tu msafara baba yao alisema: Hakika mimi nasikia harufu ya Yusuf, lau kuwa hamtanituhumu.
قَالُوا۟ تَٱللَّهِ إِنَّكَ لَفِى ضَلَٰلِكَ ٱلْقَدِيمِ
Wakasema: Wallahi! Hakika bado ungali katika upotovu wako wa zamani.
فَلَمَّآ أَن جَآءَ ٱلْبَشِيرُ أَلْقَىٰهُ عَلَىٰ وَجْهِهِۦ فَٱرْتَدَّ بَصِيرًۭا ۖ قَالَ أَلَمْ أَقُل لَّكُمْ إِنِّىٓ أَعْلَمُ مِنَ ٱللَّهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ
Basi alipo fika mbashiri na akaiweka kanzu usoni pake alirejea kuona. Akasema: Je! Sikukwambieni kuwa mimi najua ya Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi?
قَالُوا۟ يَٰٓأَبَانَا ٱسْتَغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَآ إِنَّا كُنَّا خَٰطِـِٔينَ
Wakasema: Ee baba yetu! Tuombee msamaha kwa dhambi zetu. Hapana shaka sisi tulikuwa na makosa.
قَالَ سَوْفَ أَسْتَغْفِرُ لَكُمْ رَبِّىٓ ۖ إِنَّهُۥ هُوَ ٱلْغَفُورُ ٱلرَّحِيمُ
Akasema: Nitakuja kuombeeni msamaha kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye maghfira na Mwenye kusamehe.
فَلَمَّا دَخَلُوا۟ عَلَىٰ يُوسُفَ ءَاوَىٰٓ إِلَيْهِ أَبَوَيْهِ وَقَالَ ٱدْخُلُوا۟ مِصْرَ إِن شَآءَ ٱللَّهُ ءَامِنِينَ
Na walipo ingia kwa Yusuf aliwakumbatia wazazi wake na akasema: Ingieni Misri, Inshallah, mmo katika amani.
وَرَفَعَ أَبَوَيْهِ عَلَى ٱلْعَرْشِ وَخَرُّوا۟ لَهُۥ سُجَّدًۭا ۖ وَقَالَ يَٰٓأَبَتِ هَٰذَا تَأْوِيلُ رُءْيَٰىَ مِن قَبْلُ قَدْ جَعَلَهَا رَبِّى حَقًّۭا ۖ وَقَدْ أَحْسَنَ بِىٓ إِذْ أَخْرَجَنِى مِنَ ٱلسِّجْنِ وَجَآءَ بِكُم مِّنَ ٱلْبَدْوِ مِنۢ بَعْدِ أَن نَّزَغَ ٱلشَّيْطَٰنُ بَيْنِى وَبَيْنَ إِخْوَتِىٓ ۚ إِنَّ رَبِّى لَطِيفٌۭ لِّمَا يَشَآءُ ۚ إِنَّهُۥ هُوَ ٱلْعَلِيمُ ٱلْحَكِيمُ
Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi. Na wote wakaporomoka kumsujudia. Na akasema: Ewe baba yangu! Hii ndiyo tafsiri ya ile ndoto yangu ya zamani. Na Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe kweli. Na Mwenyezi Mungu amenifanyia wema kunitoa gerezani, na kukuleteni kutoka jangwani baada ya Shet'ani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mpole kwa alitakalo. Bila ya shaka Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima.
۞ رَبِّ قَدْ ءَاتَيْتَنِى مِنَ ٱلْمُلْكِ وَعَلَّمْتَنِى مِن تَأْوِيلِ ٱلْأَحَادِيثِ ۚ فَاطِرَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ أَنتَ وَلِىِّۦ فِى ٱلدُّنْيَا وَٱلْءَاخِرَةِ ۖ تَوَفَّنِى مُسْلِمًۭا وَأَلْحِقْنِى بِٱلصَّٰلِحِينَ
Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika umenipa utawala, na umenifunza tafsiri ya mambo. Ewe Muumba wa mbingu na ardhi! Wewe ndiye Mlinzi wangu katika dunia na Akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Muislamu na nichanganyishe na watendao mema.
ذَٰلِكَ مِنْ أَنۢبَآءِ ٱلْغَيْبِ نُوحِيهِ إِلَيْكَ ۖ وَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ أَجْمَعُوٓا۟ أَمْرَهُمْ وَهُمْ يَمْكُرُونَ
Hizi ni katika khabari za ghaibu tulizo kufunulia. Na hukuwa pamoja nao walipo azimia shauri yao, walipo fanya njama zao wakizua vitimbi.
وَمَآ أَكْثَرُ ٱلنَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ
Na wengi wa watu si wenye kuamini hata ukijitahidi vipi..
وَمَا تَسْـَٔلُهُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌۭ لِّلْعَٰلَمِينَ
Wala wewe huwaombi ujira kwa haya. Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote.
وَكَأَيِّن مِّنْ ءَايَةٍۢ فِى ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ يَمُرُّونَ عَلَيْهَا وَهُمْ عَنْهَا مُعْرِضُونَ
Na ishara ngapi katika mbingu na ardhi wanazo zipitia, na hali ya kuwa wanazipuuza.
وَمَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُم بِٱللَّهِ إِلَّا وَهُم مُّشْرِكُونَ
Na wengi katika wao hawamuamini Mwenyezi Mungu pasina kuwa ni washirikina.
أَفَأَمِنُوٓا۟ أَن تَأْتِيَهُمْ غَٰشِيَةٌۭ مِّنْ عَذَابِ ٱللَّهِ أَوْ تَأْتِيَهُمُ ٱلسَّاعَةُ بَغْتَةًۭ وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ
Je! Wanaaminisha kuwa haitowajia adhabu ya Mwenyezi Mungu ya kuwagubika, au haitawafikia Saa ya Kiyama kwa ghafla, na hali hawatambui?
قُلْ هَٰذِهِۦ سَبِيلِىٓ أَدْعُوٓا۟ إِلَى ٱللَّهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا۠ وَمَنِ ٱتَّبَعَنِى ۖ وَسُبْحَٰنَ ٱللَّهِ وَمَآ أَنَا۠ مِنَ ٱلْمُشْرِكِينَ
Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua - mimi na wanao nifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.
وَمَآ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ إِلَّا رِجَالًۭا نُّوحِىٓ إِلَيْهِم مِّنْ أَهْلِ ٱلْقُرَىٰٓ ۗ أَفَلَمْ يَسِيرُوا۟ فِى ٱلْأَرْضِ فَيَنظُرُوا۟ كَيْفَ كَانَ عَٰقِبَةُ ٱلَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۗ وَلَدَارُ ٱلْءَاخِرَةِ خَيْرٌۭ لِّلَّذِينَ ٱتَّقَوْا۟ ۗ أَفَلَا تَعْقِلُونَ
Na hatukuwatuma Mitume kabla yako isipo kuwa wanaume tulio wafunulia wahyi miongoni mwa watu wa mijini. Je! Hawatembei katika ardhi wakaona jinsi ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Na hakika nyumba ya Akhera ni bora kwa wamchao Mungu. Basi hamfahamu?
حَتَّىٰٓ إِذَا ٱسْتَيْـَٔسَ ٱلرُّسُلُ وَظَنُّوٓا۟ أَنَّهُمْ قَدْ كُذِبُوا۟ جَآءَهُمْ نَصْرُنَا فَنُجِّىَ مَن نَّشَآءُ ۖ وَلَا يُرَدُّ بَأْسُنَا عَنِ ٱلْقَوْمِ ٱلْمُجْرِمِينَ
Hata Mitume walipo kata tamaa na wakaona kuwa wamekadhibishwa, hapo ikawajia nusura yetu, wakaokolewa tuwatakao. Na adhabu yetu haitowawacha kaumu ya wakosefu.
لَقَدْ كَانَ فِى قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌۭ لِّأُو۟لِى ٱلْأَلْبَٰبِ ۗ مَا كَانَ حَدِيثًۭا يُفْتَرَىٰ وَلَٰكِن تَصْدِيقَ ٱلَّذِى بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلِّ شَىْءٍۢ وَهُدًۭى وَرَحْمَةًۭ لِّقَوْمٍۢ يُؤْمِنُونَ
Kwa hakika katika hadithi zao limo zingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.

Surah 13: Ar-Ra'd — الرعد

الٓمٓر ۚ تِلْكَ ءَايَٰتُ ٱلْكِتَٰبِ ۗ وَٱلَّذِىٓ أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ٱلْحَقُّ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ ٱلنَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ
Alif Lam Mym Ra. (A. L. M. R.) Hizi ni Ishara za Kitabu. Na uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi ni Haki. Lakini wengi wa watu hawaamini.
ٱللَّهُ ٱلَّذِى رَفَعَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ بِغَيْرِ عَمَدٍۢ تَرَوْنَهَا ۖ ثُمَّ ٱسْتَوَىٰ عَلَى ٱلْعَرْشِ ۖ وَسَخَّرَ ٱلشَّمْسَ وَٱلْقَمَرَ ۖ كُلٌّۭ يَجْرِى لِأَجَلٍۢ مُّسَمًّۭى ۚ يُدَبِّرُ ٱلْأَمْرَ يُفَصِّلُ ٱلْءَايَٰتِ لَعَلَّكُم بِلِقَآءِ رَبِّكُمْ تُوقِنُونَ
Mwenyezi Mungu aliye ziinua mbingu bila ya nguzo mnazo ziona, ametawala kwenye Ufalme wake, na amefanya jua na mwezi yamt'ii, kila kimoja kinakwenda kwa kiwango maalumu. Anayapanga mambo, na anazipambanua Ishara ili mpate kuwa na yakini kukutana na Mola wenu Mlezi.
وَهُوَ ٱلَّذِى مَدَّ ٱلْأَرْضَ وَجَعَلَ فِيهَا رَوَٰسِىَ وَأَنْهَٰرًۭا ۖ وَمِن كُلِّ ٱلثَّمَرَٰتِ جَعَلَ فِيهَا زَوْجَيْنِ ٱثْنَيْنِ ۖ يُغْشِى ٱلَّيْلَ ٱلنَّهَارَ ۚ إِنَّ فِى ذَٰلِكَ لَءَايَٰتٍۢ لِّقَوْمٍۢ يَتَفَكَّرُونَ
Na ndiye aliye itandaza ardhi na akaweka humo milima na mito. Na katika kila matunda akafanya dume na jike. Huufunika usiku juu ya mchana. Hakika katika haya zimo Ishara kwa watu wanao fikiri.
وَفِى ٱلْأَرْضِ قِطَعٌۭ مُّتَجَٰوِرَٰتٌۭ وَجَنَّٰتٌۭ مِّنْ أَعْنَٰبٍۢ وَزَرْعٌۭ وَنَخِيلٌۭ صِنْوَانٌۭ وَغَيْرُ صِنْوَانٍۢ يُسْقَىٰ بِمَآءٍۢ وَٰحِدٍۢ وَنُفَضِّلُ بَعْضَهَا عَلَىٰ بَعْضٍۢ فِى ٱلْأُكُلِ ۚ إِنَّ فِى ذَٰلِكَ لَءَايَٰتٍۢ لِّقَوْمٍۢ يَعْقِلُونَ
Na katika ardhi vimo vipande vilivyo karibiana, na zipo bustani za mizabibu, na mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na isio chipua kwenye shina moja, nayo inatiliwa maji yale yale. Na tunaifanya baadhi yao bora kuliko mengine katika kula. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanao tia mambo akilini.
۞ وَإِن تَعْجَبْ فَعَجَبٌۭ قَوْلُهُمْ أَءِذَا كُنَّا تُرَٰبًا أَءِنَّا لَفِى خَلْقٍۢ جَدِيدٍ ۗ أُو۟لَٰٓئِكَ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ بِرَبِّهِمْ ۖ وَأُو۟لَٰٓئِكَ ٱلْأَغْلَٰلُ فِىٓ أَعْنَاقِهِمْ ۖ وَأُو۟لَٰٓئِكَ أَصْحَٰبُ ٱلنَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَٰلِدُونَ
Na kama ukistaajabu, basi cha ajabu zaidi ni huo usemi wao: Ati tukisha kuwa mchanga kweli tutakuwa katika umbo jipya? Hao ndio walio mkufuru Mola wao Mlezi. Na hao ndio watao kuwa na makongwa shingoni mwao, na hao ndio watu wa Motoni. Humo watadumu.
وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِٱلسَّيِّئَةِ قَبْلَ ٱلْحَسَنَةِ وَقَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِمُ ٱلْمَثُلَٰتُ ۗ وَإِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍۢ لِّلنَّاسِ عَلَىٰ ظُلْمِهِمْ ۖ وَإِنَّ رَبَّكَ لَشَدِيدُ ٱلْعِقَابِ
Na wanakuhimiza ulete maovu kabla ya mema, hali ya kuwa zimekwisha pita kabla yao adhabu za kupigiwa mfano. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye msamaha kwa watu juu ya udhalimu wao. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mkali wa kuadhibu.
وَيَقُولُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ لَوْلَآ أُنزِلَ عَلَيْهِ ءَايَةٌۭ مِّن رَّبِّهِۦٓ ۗ إِنَّمَآ أَنتَ مُنذِرٌۭ ۖ وَلِكُلِّ قَوْمٍ هَادٍ
Na wale walio kufuru husema: Mbona hakuteremshiwa muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi? Hakika wewe ni Mwonyaji, na kila kaumu ina wa kuwaongoa.
ٱللَّهُ يَعْلَمُ مَا تَحْمِلُ كُلُّ أُنثَىٰ وَمَا تَغِيضُ ٱلْأَرْحَامُ وَمَا تَزْدَادُ ۖ وَكُلُّ شَىْءٍ عِندَهُۥ بِمِقْدَارٍ
Mwenyezi Mungu anajua mimba abebayo kila mwanamke, na kinacho punguka na kuzidi matumboni. Na kila kitu kwake ni kwa kipimo.
عَٰلِمُ ٱلْغَيْبِ وَٱلشَّهَٰدَةِ ٱلْكَبِيرُ ٱلْمُتَعَالِ
Yeye ndiye Mwenye kujua yanayo onekana na yasio onekana; Mkuu Aliye tukuka.
سَوَآءٌۭ مِّنكُم مَّنْ أَسَرَّ ٱلْقَوْلَ وَمَن جَهَرَ بِهِۦ وَمَنْ هُوَ مُسْتَخْفٍۭ بِٱلَّيْلِ وَسَارِبٌۢ بِٱلنَّهَارِ
Ni sawa anaye ficha kauli yake kati yenu na anaye idhihirisha, na anaye jibanza usiku na anaye tembea jahara mchana.
لَهُۥ مُعَقِّبَٰتٌۭ مِّنۢ بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِۦ يَحْفَظُونَهُۥ مِنْ أَمْرِ ٱللَّهِ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا۟ مَا بِأَنفُسِهِمْ ۗ وَإِذَآ أَرَادَ ٱللَّهُ بِقَوْمٍۢ سُوٓءًۭا فَلَا مَرَدَّ لَهُۥ ۚ وَمَا لَهُم مِّن دُونِهِۦ مِن وَالٍ
Kila mtu analo kundi la malaika mbele yake na nyuma yake linamlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf- sini mwao. Na Mwenyezi Mungu anapo watakia watu adhabu hakuna cha kuzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake.
هُوَ ٱلَّذِى يُرِيكُمُ ٱلْبَرْقَ خَوْفًۭا وَطَمَعًۭا وَيُنشِئُ ٱلسَّحَابَ ٱلثِّقَالَ
Yeye ndiye anaye kuonyesheni umeme kwa khofu na tamaa, na huyaleta mawingu mazito.
وَيُسَبِّحُ ٱلرَّعْدُ بِحَمْدِهِۦ وَٱلْمَلَٰٓئِكَةُ مِنْ خِيفَتِهِۦ وَيُرْسِلُ ٱلصَّوَٰعِقَ فَيُصِيبُ بِهَا مَن يَشَآءُ وَهُمْ يُجَٰدِلُونَ فِى ٱللَّهِ وَهُوَ شَدِيدُ ٱلْمِحَالِ
Na radi inamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumhimidi, na Malaika pia, kwa kumkhofu. Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye. Nao wanabishana juu ya Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni Mwenye adhabu kali!
لَهُۥ دَعْوَةُ ٱلْحَقِّ ۖ وَٱلَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِۦ لَا يَسْتَجِيبُونَ لَهُم بِشَىْءٍ إِلَّا كَبَٰسِطِ كَفَّيْهِ إِلَى ٱلْمَآءِ لِيَبْلُغَ فَاهُ وَمَا هُوَ بِبَٰلِغِهِۦ ۚ وَمَا دُعَآءُ ٱلْكَٰفِرِينَ إِلَّا فِى ضَلَٰلٍۢ
Wa kuombwa kweli ni Yeye tu. Na hao wanao waomba badala yake hawawajibu chochote; bali ni kama mwenye kunyoosha viganja vyake kwenye maji ili yafike kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila katika upotovu.
وَلِلَّهِ يَسْجُدُ مَن فِى ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ طَوْعًۭا وَكَرْهًۭا وَظِلَٰلُهُم بِٱلْغُدُوِّ وَٱلْءَاصَالِ ۩
Na viliomo mbinguni na katika ardhi vinamsujudia Mwenyezi Mungu tu vikitaka visitake. Na pia vivuli vyao asubuhi na jioni.
قُلْ مَن رَّبُّ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ قُلِ ٱللَّهُ ۚ قُلْ أَفَٱتَّخَذْتُم مِّن دُونِهِۦٓ أَوْلِيَآءَ لَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ نَفْعًۭا وَلَا ضَرًّۭا ۚ قُلْ هَلْ يَسْتَوِى ٱلْأَعْمَىٰ وَٱلْبَصِيرُ أَمْ هَلْ تَسْتَوِى ٱلظُّلُمَٰتُ وَٱلنُّورُ ۗ أَمْ جَعَلُوا۟ لِلَّهِ شُرَكَآءَ خَلَقُوا۟ كَخَلْقِهِۦ فَتَشَٰبَهَ ٱلْخَلْقُ عَلَيْهِمْ ۚ قُلِ ٱللَّهُ خَٰلِقُ كُلِّ شَىْءٍۢ وَهُوَ ٱلْوَٰحِدُ ٱلْقَهَّٰرُ
Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu na ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, mnawafanya wenginewe badala yake kuwa ni walinzi, nao hawajifai wenyewe kwa jema wala baya? Sema: Hebu kipofu na mwenye kuona huwa sawa? Au hebu huwa sawa giza na mwangaza? Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika walio umba kama alivyo umba Yeye, na viumbe hivyo vikawadanganyikia? Sema: Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na Yeye ni Mmoja Mwenye kushinda!
أَنزَلَ مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءًۭ فَسَالَتْ أَوْدِيَةٌۢ بِقَدَرِهَا فَٱحْتَمَلَ ٱلسَّيْلُ زَبَدًۭا رَّابِيًۭا ۚ وَمِمَّا يُوقِدُونَ عَلَيْهِ فِى ٱلنَّارِ ٱبْتِغَآءَ حِلْيَةٍ أَوْ مَتَٰعٍۢ زَبَدٌۭ مِّثْلُهُۥ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ ٱللَّهُ ٱلْحَقَّ وَٱلْبَٰطِلَ ۚ فَأَمَّا ٱلزَّبَدُ فَيَذْهَبُ جُفَآءًۭ ۖ وَأَمَّا مَا يَنفَعُ ٱلنَّاسَ فَيَمْكُثُ فِى ٱلْأَرْضِ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ ٱللَّهُ ٱلْأَمْثَالَ
Ameteremsha maji kutoka mbinguni. Na mabonde yakamiminika maji kwa kadiri yake. Na mafuriko yakachukua mapovu yaliyo kusanyika juu yake. Na kutokana na wanavyo yayusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo hutokea povu vile vile. Namna hivyo Mwenyezi Mungu ndivyo anavyo piga mifano ya Haki na baat'ili. Basi lile povu linapita kama takataka tu basi. Ama kinacho wafaa watu hubakia kwenye ardhi. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga mifano.
لِلَّذِينَ ٱسْتَجَابُوا۟ لِرَبِّهِمُ ٱلْحُسْنَىٰ ۚ وَٱلَّذِينَ لَمْ يَسْتَجِيبُوا۟ لَهُۥ لَوْ أَنَّ لَهُم مَّا فِى ٱلْأَرْضِ جَمِيعًۭا وَمِثْلَهُۥ مَعَهُۥ لَٱفْتَدَوْا۟ بِهِۦٓ ۚ أُو۟لَٰٓئِكَ لَهُمْ سُوٓءُ ٱلْحِسَابِ وَمَأْوَىٰهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ ٱلْمِهَادُ
Walio muitikia Mola wao Mlezi watapata wema. Na wasio muitikia, hata wangeli kuwa navyo vyote viliomo katika ardhi na mfano wa hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa kujikombolea! Hao watapata hisabu mbaya kabisa, na makao yao ni Jahannamu. Na hapo ni pahala pabaya mno!
۞ أَفَمَن يَعْلَمُ أَنَّمَآ أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ٱلْحَقُّ كَمَنْ هُوَ أَعْمَىٰٓ ۚ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُو۟لُوا۟ ٱلْأَلْبَٰبِ
Je! Anaye jua ya kwamba yaliyo teremshwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi ni Haki ni sawa na aliye kipofu? Wenye akili ndio wanao zingatia,
ٱلَّذِينَ يُوفُونَ بِعَهْدِ ٱللَّهِ وَلَا يَنقُضُونَ ٱلْمِيثَٰقَ
Wale ambao wanatimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu, wala hawavunji maagano.
وَٱلَّذِينَ يَصِلُونَ مَآ أَمَرَ ٱللَّهُ بِهِۦٓ أَن يُوصَلَ وَيَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ وَيَخَافُونَ سُوٓءَ ٱلْحِسَابِ
Na wale ambao huyaunga aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanaikhofu hisabu mbaya.
وَٱلَّذِينَ صَبَرُوا۟ ٱبْتِغَآءَ وَجْهِ رَبِّهِمْ وَأَقَامُوا۟ ٱلصَّلَوٰةَ وَأَنفَقُوا۟ مِمَّا رَزَقْنَٰهُمْ سِرًّۭا وَعَلَانِيَةًۭ وَيَدْرَءُونَ بِٱلْحَسَنَةِ ٱلسَّيِّئَةَ أُو۟لَٰٓئِكَ لَهُمْ عُقْبَى ٱلدَّارِ
Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao Mlezi, na wakashika Sala, na wakatoa, kwa siri na kwa uwazi, katika tulivyo wapa; na wakayaondoa maovu kwa wema. Hao ndio watakao pata malipo ya Nyumba ya Akhera.
جَنَّٰتُ عَدْنٍۢ يَدْخُلُونَهَا وَمَن صَلَحَ مِنْ ءَابَآئِهِمْ وَأَزْوَٰجِهِمْ وَذُرِّيَّٰتِهِمْ ۖ وَٱلْمَلَٰٓئِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍۢ
Nayo ni Bustani za milele, wataziingia wao na walio wema miongoni mwa baba zao, na wake zao, na vizazi vyao. Na Malaika wanawaingilia katika kila mlango.
سَلَٰمٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ ۚ فَنِعْمَ عُقْبَى ٱلدَّارِ
(Wakiwaambia) Assalamu Alaikum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyo subiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera.
وَٱلَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ ٱللَّهِ مِنۢ بَعْدِ مِيثَٰقِهِۦ وَيَقْطَعُونَ مَآ أَمَرَ ٱللَّهُ بِهِۦٓ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِى ٱلْأَرْضِ ۙ أُو۟لَٰٓئِكَ لَهُمُ ٱللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوٓءُ ٱلدَّارِ
Na wale wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuzifunga, na wanakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya fisadi katika nchi: hao ndio watakao pata laana, na watapata Nyumba mbaya.
ٱللَّهُ يَبْسُطُ ٱلرِّزْقَ لِمَن يَشَآءُ وَيَقْدِرُ ۚ وَفَرِحُوا۟ بِٱلْحَيَوٰةِ ٱلدُّنْيَا وَمَا ٱلْحَيَوٰةُ ٱلدُّنْيَا فِى ٱلْءَاخِرَةِ إِلَّا مَتَٰعٌۭ
Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humkunjia kwa kipimo. Na wamefurahia maisha ya dunia. Na uhai wa dunia kwa kulingana na Akhera si kitu ila ni starehe ndogo.
وَيَقُولُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ لَوْلَآ أُنزِلَ عَلَيْهِ ءَايَةٌۭ مِّن رَّبِّهِۦ ۗ قُلْ إِنَّ ٱللَّهَ يُضِلُّ مَن يَشَآءُ وَيَهْدِىٓ إِلَيْهِ مَنْ أَنَابَ
Na wanasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu humwacha kupotea amtakaye, na humwongoa anaye elekea kwake,
ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ ٱللَّهِ ۗ أَلَا بِذِكْرِ ٱللَّهِ تَطْمَئِنُّ ٱلْقُلُوبُ
Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua!
ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّٰلِحَٰتِ طُوبَىٰ لَهُمْ وَحُسْنُ مَـَٔابٍۢ
Wale walio amini na wakatenda mema watakuwa na raha na marejeo mazuri.
كَذَٰلِكَ أَرْسَلْنَٰكَ فِىٓ أُمَّةٍۢ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهَآ أُمَمٌۭ لِّتَتْلُوَا۟ عَلَيْهِمُ ٱلَّذِىٓ أَوْحَيْنَآ إِلَيْكَ وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِٱلرَّحْمَٰنِ ۚ قُلْ هُوَ رَبِّى لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ مَتَابِ
Ndio kama hivi tumekutuma kwa umma ambao wamekwsiha pita kabla yao umati nyengine, ili uwasomee tunayo kufunulia, na wao wanamkufuru Rahmani, Mwingi wa Rehema! Sema: Yeye ndiye Mola wangu Mlezi. Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Juu yake nimetegemea, na kwake ndio marejeo yangu!
وَلَوْ أَنَّ قُرْءَانًۭا سُيِّرَتْ بِهِ ٱلْجِبَالُ أَوْ قُطِّعَتْ بِهِ ٱلْأَرْضُ أَوْ كُلِّمَ بِهِ ٱلْمَوْتَىٰ ۗ بَل لِّلَّهِ ٱلْأَمْرُ جَمِيعًا ۗ أَفَلَمْ يَا۟يْـَٔسِ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓا۟ أَن لَّوْ يَشَآءُ ٱللَّهُ لَهَدَى ٱلنَّاسَ جَمِيعًۭا ۗ وَلَا يَزَالُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ تُصِيبُهُم بِمَا صَنَعُوا۟ قَارِعَةٌ أَوْ تَحُلُّ قَرِيبًۭا مِّن دَارِهِمْ حَتَّىٰ يَأْتِىَ وَعْدُ ٱللَّهِ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يُخْلِفُ ٱلْمِيعَادَ
Na kama ingeli kuwako Qur'ani ndiyo inayo endeshewa milima, na kupasuliwa ardhi, na kusemeshewa wafu, (basi ingeli kuwa Qur'ani hii). Bali mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Je, hawajajua walio amini kwamba lau kuwa Mwenyezi Mungu ange penda bila ya shaka angeli waongoa watu wote? Wala walio kufuru hawaachi kusibiwa na balaa kwa waliyo yatenda, au ikawateremkia karibu na nyumbani kwao, mpaka ifike ahadi ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi yake.
وَلَقَدِ ٱسْتُهْزِئَ بِرُسُلٍۢ مِّن قَبْلِكَ فَأَمْلَيْتُ لِلَّذِينَ كَفَرُوا۟ ثُمَّ أَخَذْتُهُمْ ۖ فَكَيْفَ كَانَ عِقَابِ
Na hakika walifanyiwa kejeli Mitume walio kuwa kabla yako. Na nikawapururia wale walio kufuru, kisha nikawashika! Basi ilikuwaje adhabu yangu!
أَفَمَنْ هُوَ قَآئِمٌ عَلَىٰ كُلِّ نَفْسٍۭ بِمَا كَسَبَتْ ۗ وَجَعَلُوا۟ لِلَّهِ شُرَكَآءَ قُلْ سَمُّوهُمْ ۚ أَمْ تُنَبِّـُٔونَهُۥ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِى ٱلْأَرْضِ أَم بِظَٰهِرٍۢ مِّنَ ٱلْقَوْلِ ۗ بَلْ زُيِّنَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا۟ مَكْرُهُمْ وَصُدُّوا۟ عَنِ ٱلسَّبِيلِ ۗ وَمَن يُضْلِلِ ٱللَّهُ فَمَا لَهُۥ مِنْ هَادٍۢ
Je! Anaye isimamia kila nafsi kwa yale iliyo yachuma...? Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu kuwa na washirika! Sema watajeni. Au ndio mnampa khabari ya yale asiyo yajua katika ardhi; au ni maneno matupu? Bali walio kufuru wamepambiwa vitimbi vyao na wamezuiliwa njia. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha apotee basi hana wa kumwongoa.
لَّهُمْ عَذَابٌۭ فِى ٱلْحَيَوٰةِ ٱلدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ ٱلْءَاخِرَةِ أَشَقُّ ۖ وَمَا لَهُم مِّنَ ٱللَّهِ مِن وَاقٍۢ
Wanayo adhabu katika maisha ya dunia, na adhabu ya Akhera hapana shaka ina mashaka zaidi. Na wala hawatakuwa na wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu.
۞ مَّثَلُ ٱلْجَنَّةِ ٱلَّتِى وُعِدَ ٱلْمُتَّقُونَ ۖ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَٰرُ ۖ أُكُلُهَا دَآئِمٌۭ وَظِلُّهَا ۚ تِلْكَ عُقْبَى ٱلَّذِينَ ٱتَّقَوا۟ ۖ وَّعُقْبَى ٱلْكَٰفِرِينَ ٱلنَّارُ
Mfano wa Bustani waliyo ahidiwa wachamngu, kati yake inapita mito, matunda yake ni ya daima, na pia kivuli chake. Huu ndio mwisho wa wale walio walio jilinda. Na mwisho wa makafiri ni Moto.
وَٱلَّذِينَ ءَاتَيْنَٰهُمُ ٱلْكِتَٰبَ يَفْرَحُونَ بِمَآ أُنزِلَ إِلَيْكَ ۖ وَمِنَ ٱلْأَحْزَابِ مَن يُنكِرُ بَعْضَهُۥ ۚ قُلْ إِنَّمَآ أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ ٱللَّهَ وَلَآ أُشْرِكَ بِهِۦٓ ۚ إِلَيْهِ أَدْعُوا۟ وَإِلَيْهِ مَـَٔابِ
Na tulio wapa Kitabu wanafurahia uliyo teremshiwa. Na katika makundi mengine wapo wanao yakataa baadhi ya haya. Sema: Nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu, na wala nisimshirikishe. Kuendea kwake Yeye ndiyo ninaita, na kwake Yeye ndio marejeo yangu.
وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَٰهُ حُكْمًا عَرَبِيًّۭا ۚ وَلَئِنِ ٱتَّبَعْتَ أَهْوَآءَهُم بَعْدَمَا جَآءَكَ مِنَ ٱلْعِلْمِ مَا لَكَ مِنَ ٱللَّهِ مِن وَلِىٍّۢ وَلَا وَاقٍۢ
Na ndio kama hivi tumeiteremsha Qur'ani kuwa ni hukumu kwa lugha ya Kiarabu. Na ukifuata matamanio yao baada ya kukujia ilimu hii, hutakuwa na rafiki wala mlinzi mbele ya Mwenyezi Mungu.
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًۭا مِّن قَبْلِكَ وَجَعَلْنَا لَهُمْ أَزْوَٰجًۭا وَذُرِّيَّةًۭ ۚ وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَن يَأْتِىَ بِـَٔايَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ ٱللَّهِ ۗ لِكُلِّ أَجَلٍۢ كِتَابٌۭ
Na hakika Sisi tulikwisha watuma Mitume kabla yako, na tukajaalia wawe na wake na dhuriya. Na haiwi kwa Mtume kuleta miujiza isipo kuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila kipindi kina hukumu yake.
يَمْحُوا۟ ٱللَّهُ مَا يَشَآءُ وَيُثْبِتُ ۖ وَعِندَهُۥٓ أُمُّ ٱلْكِتَٰبِ
Mwenyezi Mungu hufuta na huthibitisha ayatakayo. Na asili ya hukumu zote iko kwake.
وَإِن مَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ ٱلَّذِى نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِنَّمَا عَلَيْكَ ٱلْبَلَٰغُ وَعَلَيْنَا ٱلْحِسَابُ
Na ikiwa tukikuonyesha baadhi ya tuliyo waahidi au tukakufisha kabla yake, juu yako wewe ni kufikisha ujumbe na juu yetu ni hisabu.
أَوَلَمْ يَرَوْا۟ أَنَّا نَأْتِى ٱلْأَرْضَ نَنقُصُهَا مِنْ أَطْرَافِهَا ۚ وَٱللَّهُ يَحْكُمُ لَا مُعَقِّبَ لِحُكْمِهِۦ ۚ وَهُوَ سَرِيعُ ٱلْحِسَابِ
Je! Hawakuona kwamba tunaifikia ardhi tukiipunguza nchani mwake? Na Mwenyezi Mungu huhukumu, na hapana wa kupinga hukumu yake, naye ni Mwepesi wa kuhisabu.
وَقَدْ مَكَرَ ٱلَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلِلَّهِ ٱلْمَكْرُ جَمِيعًۭا ۖ يَعْلَمُ مَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍۢ ۗ وَسَيَعْلَمُ ٱلْكُفَّٰرُ لِمَنْ عُقْبَى ٱلدَّارِ
Na walipanga walio kuwa kabla yao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye mipango yote. Yeye anajua inayo chuma kila nafsi. Na makafiri watajua ni ya nani nyumba ya mwisho Akhera!
وَيَقُولُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ لَسْتَ مُرْسَلًۭا ۚ قُلْ كَفَىٰ بِٱللَّهِ شَهِيدًۢا بَيْنِى وَبَيْنَكُمْ وَمَنْ عِندَهُۥ عِلْمُ ٱلْكِتَٰبِ
Na walio kufuru wanasema: Wewe hukutumwa. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi, na pia yule mwenye ilimu ya Kitabu.

Surah 14: Ibrahim — إبراهيم

الٓر ۚ كِتَٰبٌ أَنزَلْنَٰهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ ٱلنَّاسَ مِنَ ٱلظُّلُمَٰتِ إِلَى ٱلنُّورِ بِإِذْنِ رَبِّهِمْ إِلَىٰ صِرَٰطِ ٱلْعَزِيزِ ٱلْحَمِيدِ
Alif Lam Ra. (A. L. R.) Hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha kwako ili uwatowe watu kwenye giza uwapeleke kwenye muwangaza, kwa idhini ya Mola wao Mlezi, uwafikishe kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifiwa,
ٱللَّهِ ٱلَّذِى لَهُۥ مَا فِى ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَمَا فِى ٱلْأَرْضِ ۗ وَوَيْلٌۭ لِّلْكَٰفِرِينَ مِنْ عَذَابٍۢ شَدِيدٍ
Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye vyote viliomo katika mbingu na ardhi. Na ole wao makafiri kwa adhabu kali!
ٱلَّذِينَ يَسْتَحِبُّونَ ٱلْحَيَوٰةَ ٱلدُّنْيَا عَلَى ٱلْءَاخِرَةِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ ٱللَّهِ وَيَبْغُونَهَا عِوَجًا ۚ أُو۟لَٰٓئِكَ فِى ضَلَٰلٍۭ بَعِيدٍۢ
Wale wanao fadhilisha maisha ya dunia kuliko Akhera, na wanawazuilia watu wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotosha. Hao wamepotelea mbali.
وَمَآ أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِۦ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ ۖ فَيُضِلُّ ٱللَّهُ مَن يَشَآءُ وَيَهْدِى مَن يَشَآءُ ۚ وَهُوَ ٱلْعَزِيزُ ٱلْحَكِيمُ
Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa kaumu yake ili apate kuwabainishia. Basi Mwenyezi Mungu humuacha akapotea amtakaye, na akamwongoa amtakaye. Naye ni Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ بِـَٔايَٰتِنَآ أَنْ أَخْرِجْ قَوْمَكَ مِنَ ٱلظُّلُمَٰتِ إِلَى ٱلنُّورِ وَذَكِّرْهُم بِأَيَّىٰمِ ٱللَّهِ ۚ إِنَّ فِى ذَٰلِكَ لَءَايَٰتٍۢ لِّكُلِّ صَبَّارٍۢ شَكُورٍۢ
Na tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu, tukamwambia: Watoe watu wako kwenye giza uwapeleke kwenye mwangaza. Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.
وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ ٱذْكُرُوا۟ نِعْمَةَ ٱللَّهِ عَلَيْكُمْ إِذْ أَنجَىٰكُم مِّنْ ءَالِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوٓءَ ٱلْعَذَابِ وَيُذَبِّحُونَ أَبْنَآءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَآءَكُمْ ۚ وَفِى ذَٰلِكُم بَلَآءٌۭ مِّن رَّبِّكُمْ عَظِيمٌۭ
Na Musa alipo waambia watu wake: Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu aliyo kujaalieni, pale alipo kuokoeni kutokana na watu wa Firauni walio kupeni adhabu mbaya kabisa, wakiwachinja wenenu wanaume, na wakiwawacha hai wanawake. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unao toka kwa Mola wenu Mlezi.
وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِى لَشَدِيدٌۭ
Na alipo tangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.
وَقَالَ مُوسَىٰٓ إِن تَكْفُرُوٓا۟ أَنتُمْ وَمَن فِى ٱلْأَرْضِ جَمِيعًۭا فَإِنَّ ٱللَّهَ لَغَنِىٌّ حَمِيدٌ
Na Musa alisema: Mkikufuru nyinyi na wote waliomo duniani, hakika Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Anajitosha, Msifiwa.
أَلَمْ يَأْتِكُمْ نَبَؤُا۟ ٱلَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ قَوْمِ نُوحٍۢ وَعَادٍۢ وَثَمُودَ ۛ وَٱلَّذِينَ مِنۢ بَعْدِهِمْ ۛ لَا يَعْلَمُهُمْ إِلَّا ٱللَّهُ ۚ جَآءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِٱلْبَيِّنَٰتِ فَرَدُّوٓا۟ أَيْدِيَهُمْ فِىٓ أَفْوَٰهِهِمْ وَقَالُوٓا۟ إِنَّا كَفَرْنَا بِمَآ أُرْسِلْتُم بِهِۦ وَإِنَّا لَفِى شَكٍّۢ مِّمَّا تَدْعُونَنَآ إِلَيْهِ مُرِيبٍۢ
Je! Hazikukufikieni khabari za walio kabla yenu? Kaumu ya Nuhu, na A'adi, na Thamud, na walio baada yao, ambao hapana awajuaye ila Mwenyezi Mungu? Mitume wao waliwajia kwa hoja zilizo wazi, na wao wakarudisha mikono yao kwenye vinywa vyao, wakasema: Hakika sisi tumeyakataa hayo mliyo tumwa, na hakika sisi tuna shaka kubwa na mnayo tuitia.
۞ قَالَتْ رُسُلُهُمْ أَفِى ٱللَّهِ شَكٌّۭ فَاطِرِ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ ۖ يَدْعُوكُمْ لِيَغْفِرَ لَكُم مِّن ذُنُوبِكُمْ وَيُؤَخِّرَكُمْ إِلَىٰٓ أَجَلٍۢ مُّسَمًّۭى ۚ قَالُوٓا۟ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا بَشَرٌۭ مِّثْلُنَا تُرِيدُونَ أَن تَصُدُّونَا عَمَّا كَانَ يَعْبُدُ ءَابَآؤُنَا فَأْتُونَا بِسُلْطَٰنٍۢ مُّبِينٍۢ
Mitume wao wakasema: Ati pana shaka na Mwenyezi Mungu, Muumba mbingu na ardhi? Yeye anakuiteni apate kukufutieni madhambi yenu, na akupeni muhula mpaka muda ulio wekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni wanaadamu kama sisi. Mnataka kutuzuilia na waliyo kuwa wakiabudu baba zetu. Basi tuleteeni hoja ilio wazi.
قَالَتْ لَهُمْ رُسُلُهُمْ إِن نَّحْنُ إِلَّا بَشَرٌۭ مِّثْلُكُمْ وَلَٰكِنَّ ٱللَّهَ يَمُنُّ عَلَىٰ مَن يَشَآءُ مِنْ عِبَادِهِۦ ۖ وَمَا كَانَ لَنَآ أَن نَّأْتِيَكُم بِسُلْطَٰنٍ إِلَّا بِإِذْنِ ٱللَّهِ ۚ وَعَلَى ٱللَّهِ فَلْيَتَوَكَّلِ ٱلْمُؤْمِنُونَ
Mitume wao wakawaambia: Sisi kweli si chochote ila ni wanaadamu kama nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu humfanyia hisani amtakaye katika waja wake. Wala sisi hatuwezi kuleta uthibitisho ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na juu ya Mwenyezi Mungu ndio wategemee Waumini.
وَمَا لَنَآ أَلَّا نَتَوَكَّلَ عَلَى ٱللَّهِ وَقَدْ هَدَىٰنَا سُبُلَنَا ۚ وَلَنَصْبِرَنَّ عَلَىٰ مَآ ءَاذَيْتُمُونَا ۚ وَعَلَى ٱللَّهِ فَلْيَتَوَكَّلِ ٱلْمُتَوَكِّلُونَ
Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ametuongoa kwenye Njia zetu. Na hapana shaka sisi tutayavumilia hayo maudhi mnayo tuudhi. Na juu ya Mwenyezi Mungu wategemee wanao tegemea.
وَقَالَ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ لِرُسُلِهِمْ لَنُخْرِجَنَّكُم مِّنْ أَرْضِنَآ أَوْ لَتَعُودُنَّ فِى مِلَّتِنَا ۖ فَأَوْحَىٰٓ إِلَيْهِمْ رَبُّهُمْ لَنُهْلِكَنَّ ٱلظَّٰلِمِينَ
Na walio kufuru wakawaambia Mitume wao: Tutakutoeni katika nchi yetu, au mrudi katika mila yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwaletea wahyi: Hakika tutawaangamiza walio dhulumu!
وَلَنُسْكِنَنَّكُمُ ٱلْأَرْضَ مِنۢ بَعْدِهِمْ ۚ ذَٰلِكَ لِمَنْ خَافَ مَقَامِى وَخَافَ وَعِيدِ
Na tutakuwekeni katika ardhi baada yao. Haya ni kwa anaye ogopa kusimamishwa mbele yangu, na akaogopa maonyo yangu.
وَٱسْتَفْتَحُوا۟ وَخَابَ كُلُّ جَبَّارٍ عَنِيدٍۢ
Na wakaomba ushindi, na akashindwa kila jabari mkaidi,
مِّن وَرَآئِهِۦ جَهَنَّمُ وَيُسْقَىٰ مِن مَّآءٍۢ صَدِيدٍۢ
Ambaye nyuma yake ipo Jahannamu, na atanywishwa maji ya usaha.
يَتَجَرَّعُهُۥ وَلَا يَكَادُ يُسِيغُهُۥ وَيَأْتِيهِ ٱلْمَوْتُ مِن كُلِّ مَكَانٍۢ وَمَا هُوَ بِمَيِّتٍۢ ۖ وَمِن وَرَآئِهِۦ عَذَابٌ غَلِيظٌۭ
Awe anayagugumia, wala hawezi kuyameza. Na mauti yawe yanamjia kutoka kila upande, naye wala hafi. Na zaidi ya hayo ipo adhabu nyengine kali vile vile.
مَّثَلُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ بِرَبِّهِمْ ۖ أَعْمَٰلُهُمْ كَرَمَادٍ ٱشْتَدَّتْ بِهِ ٱلرِّيحُ فِى يَوْمٍ عَاصِفٍۢ ۖ لَّا يَقْدِرُونَ مِمَّا كَسَبُوا۟ عَلَىٰ شَىْءٍۢ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ ٱلضَّلَٰلُ ٱلْبَعِيدُ
Mfano wa walio mkufuru Mola wao Mlezi - vitendo vyao ni kama jivu linalo peperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya mdharba. Hawawezi kupata chochote katika waliyo yafanya. Huko ndiko kupotelea mbali!
أَلَمْ تَرَ أَنَّ ٱللَّهَ خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضَ بِٱلْحَقِّ ۚ إِن يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ وَيَأْتِ بِخَلْقٍۢ جَدِيدٍۢ
Huoni kuwa Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa Haki? Akitaka atakuondoeni na alete viumbe wapya!
وَمَا ذَٰلِكَ عَلَى ٱللَّهِ بِعَزِيزٍۢ
Na hilo kwa Mwenyezi Mungu si jambo gumu.
وَبَرَزُوا۟ لِلَّهِ جَمِيعًۭا فَقَالَ ٱلضُّعَفَٰٓؤُا۟ لِلَّذِينَ ٱسْتَكْبَرُوٓا۟ إِنَّا كُنَّا لَكُمْ تَبَعًۭا فَهَلْ أَنتُم مُّغْنُونَ عَنَّا مِنْ عَذَابِ ٱللَّهِ مِن شَىْءٍۢ ۚ قَالُوا۟ لَوْ هَدَىٰنَا ٱللَّهُ لَهَدَيْنَٰكُمْ ۖ سَوَآءٌ عَلَيْنَآ أَجَزِعْنَآ أَمْ صَبَرْنَا مَا لَنَا مِن مَّحِيصٍۢ
Na wote watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanyonge watawaambia walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi katika adhabu ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Lau Mwenyezi Mungu angeli tuongoa basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu tukipapatika au tukisubiri; hatuna pa kukimbilia.
وَقَالَ ٱلشَّيْطَٰنُ لَمَّا قُضِىَ ٱلْأَمْرُ إِنَّ ٱللَّهَ وَعَدَكُمْ وَعْدَ ٱلْحَقِّ وَوَعَدتُّكُمْ فَأَخْلَفْتُكُمْ ۖ وَمَا كَانَ لِىَ عَلَيْكُم مِّن سُلْطَٰنٍ إِلَّآ أَن دَعَوْتُكُمْ فَٱسْتَجَبْتُمْ لِى ۖ فَلَا تَلُومُونِى وَلُومُوٓا۟ أَنفُسَكُم ۖ مَّآ أَنَا۠ بِمُصْرِخِكُمْ وَمَآ أَنتُم بِمُصْرِخِىَّ ۖ إِنِّى كَفَرْتُ بِمَآ أَشْرَكْتُمُونِ مِن قَبْلُ ۗ إِنَّ ٱلظَّٰلِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌۭ
Na Shet'ani atasema itapo katwa hukumu: Hakika Mwenyezi Mungu alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini sikukutimizieni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha na Mwenyezi Mungu. Hakika madhaalimu watakuwa na adhabu chungu.
وَأُدْخِلَ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّٰلِحَٰتِ جَنَّٰتٍۢ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَٰرُ خَٰلِدِينَ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِمْ ۖ تَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَٰمٌ
Na walio amini na wakatenda mema wataingizwa katika Mabustani yapitayo mito kati yake, wadumu humo kwa idhini ya Mola wao Mlezi. Maamkio yao humo yatakuwa: Salaam!
أَلَمْ تَرَ كَيْفَ ضَرَبَ ٱللَّهُ مَثَلًۭا كَلِمَةًۭ طَيِّبَةًۭ كَشَجَرَةٍۢ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌۭ وَفَرْعُهَا فِى ٱلسَّمَآءِ
Hebu hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyo piga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni.
تُؤْتِىٓ أُكُلَهَا كُلَّ حِينٍۭ بِإِذْنِ رَبِّهَا ۗ وَيَضْرِبُ ٱللَّهُ ٱلْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ
Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.
وَمَثَلُ كَلِمَةٍ خَبِيثَةٍۢ كَشَجَرَةٍ خَبِيثَةٍ ٱجْتُثَّتْ مِن فَوْقِ ٱلْأَرْضِ مَا لَهَا مِن قَرَارٍۢ
Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, ulio ng'olewa juu ya ardhi. Hauna imara.
يُثَبِّتُ ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ بِٱلْقَوْلِ ٱلثَّابِتِ فِى ٱلْحَيَوٰةِ ٱلدُّنْيَا وَفِى ٱلْءَاخِرَةِ ۖ وَيُضِلُّ ٱللَّهُ ٱلظَّٰلِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ ٱللَّهُ مَا يَشَآءُ
Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
۞ أَلَمْ تَرَ إِلَى ٱلَّذِينَ بَدَّلُوا۟ نِعْمَتَ ٱللَّهِ كُفْرًۭا وَأَحَلُّوا۟ قَوْمَهُمْ دَارَ ٱلْبَوَارِ
Hebu hukuwaona wale walio badilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa kufuru, na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamizo?
جَهَنَّمَ يَصْلَوْنَهَا ۖ وَبِئْسَ ٱلْقَرَارُ
Nayo ni Jahannamu! Maovu yaliyoje makaazi hayo!
وَجَعَلُوا۟ لِلَّهِ أَندَادًۭا لِّيُضِلُّوا۟ عَن سَبِيلِهِۦ ۗ قُلْ تَمَتَّعُوا۟ فَإِنَّ مَصِيرَكُمْ إِلَى ٱلنَّارِ
Na walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili wapoteze watu kwenye Njia yake. Sema: Stareheni! Kwani marejeo yenu ni Motoni!
قُل لِّعِبَادِىَ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ يُقِيمُوا۟ ٱلصَّلَوٰةَ وَيُنفِقُوا۟ مِمَّا رَزَقْنَٰهُمْ سِرًّۭا وَعَلَانِيَةًۭ مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِىَ يَوْمٌۭ لَّا بَيْعٌۭ فِيهِ وَلَا خِلَٰلٌ
Waambie waja wangu walio amini, washike Sala, na watoe katika tulivyo waruzuku, kwa siri na dhaahiri, kabla haijafika Siku isiyo kuwa na biashara wala urafiki.
ٱللَّهُ ٱلَّذِى خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضَ وَأَنزَلَ مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءًۭ فَأَخْرَجَ بِهِۦ مِنَ ٱلثَّمَرَٰتِ رِزْقًۭا لَّكُمْ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ ٱلْفُلْكَ لِتَجْرِىَ فِى ٱلْبَحْرِ بِأَمْرِهِۦ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ ٱلْأَنْهَٰرَ
Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akateremsha maji kutoka mbinguni. Na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni riziki yenu. Na akafanya yakutumikieni majahazi yanayo pita baharini kwa amri yake, na akaifanya mito ikutumikieni.
وَسَخَّرَ لَكُمُ ٱلشَّمْسَ وَٱلْقَمَرَ دَآئِبَيْنِ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ ٱلَّيْلَ وَٱلنَّهَارَ
Na akalifanya jua na mwezi kwa manufaa yenu daima dawamu, na akaufanya usiku na mchana kwa manufaa yenu.
وَءَاتَىٰكُم مِّن كُلِّ مَا سَأَلْتُمُوهُ ۚ وَإِن تَعُدُّوا۟ نِعْمَتَ ٱللَّهِ لَا تُحْصُوهَآ ۗ إِنَّ ٱلْإِنسَٰنَ لَظَلُومٌۭ كَفَّارٌۭ
Na akakupeni kila mlicho muomba. Na mkihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamwezi kuzidhibiti. Hakika mwanaadamu ni dhaalimu mkubwa, mwenye kuzikufuru neema.
وَإِذْ قَالَ إِبْرَٰهِيمُ رَبِّ ٱجْعَلْ هَٰذَا ٱلْبَلَدَ ءَامِنًۭا وَٱجْنُبْنِى وَبَنِىَّ أَن نَّعْبُدَ ٱلْأَصْنَامَ
Na Ibrahim alipo sema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ujaalie mji huu uwe wa amani, na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu.
رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًۭا مِّنَ ٱلنَّاسِ ۖ فَمَن تَبِعَنِى فَإِنَّهُۥ مِنِّى ۖ وَمَنْ عَصَانِى فَإِنَّكَ غَفُورٌۭ رَّحِيمٌۭ
Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hayo yamewapoteza watu wengi. Basi aliye nifuata mimi huyo ni wangu, na aliye niasi, hakika Wewe ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
رَّبَّنَآ إِنِّىٓ أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِى بِوَادٍ غَيْرِ ذِى زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ ٱلْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُوا۟ ٱلصَّلَوٰةَ فَٱجْعَلْ أَفْـِٔدَةًۭ مِّنَ ٱلنَّاسِ تَهْوِىٓ إِلَيْهِمْ وَٱرْزُقْهُم مِّنَ ٱلثَّمَرَٰتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ
Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba yako Takatifu, ewe Mola wetu Mlezi, ili washike Sala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na waruzuku matunda, ili wapata kushukuru.
رَبَّنَآ إِنَّكَ تَعْلَمُ مَا نُخْفِى وَمَا نُعْلِنُ ۗ وَمَا يَخْفَىٰ عَلَى ٱللَّهِ مِن شَىْءٍۢ فِى ٱلْأَرْضِ وَلَا فِى ٱلسَّمَآءِ
Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe unajua tunayo yaficha na tunayo yatangaza. Na hapana kitu kinacho fichikana kwa Mwenyezi Mungu katika ardhi wala katika mbingu.
ٱلْحَمْدُ لِلَّهِ ٱلَّذِى وَهَبَ لِى عَلَى ٱلْكِبَرِ إِسْمَٰعِيلَ وَإِسْحَٰقَ ۚ إِنَّ رَبِّى لَسَمِيعُ ٱلدُّعَآءِ
Alhamdulillahi! Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu aliye nipa juu ya uzee wangu Ismail na Is-haq. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusikia maombi.
رَبِّ ٱجْعَلْنِى مُقِيمَ ٱلصَّلَوٰةِ وَمِن ذُرِّيَّتِى ۚ رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَآءِ
Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Sala, na katika dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee dua yangu.
رَبَّنَا ٱغْفِرْ لِى وَلِوَٰلِدَىَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ ٱلْحِسَابُ
Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu.
وَلَا تَحْسَبَنَّ ٱللَّهَ غَٰفِلًا عَمَّا يَعْمَلُ ٱلظَّٰلِمُونَ ۚ إِنَّمَا يُؤَخِّرُهُمْ لِيَوْمٍۢ تَشْخَصُ فِيهِ ٱلْأَبْصَٰرُ
Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayo yafanya madhaalimu. Hakika Yeye anawaakhirisha tu mpaka siku yatapo kodoka macho yao.
مُهْطِعِينَ مُقْنِعِى رُءُوسِهِمْ لَا يَرْتَدُّ إِلَيْهِمْ طَرْفُهُمْ ۖ وَأَفْـِٔدَتُهُمْ هَوَآءٌۭ
Nao wako mbioni, vichwa juu, na macho hayapepesi, na nyoyo zao tupu.
وَأَنذِرِ ٱلنَّاسَ يَوْمَ يَأْتِيهِمُ ٱلْعَذَابُ فَيَقُولُ ٱلَّذِينَ ظَلَمُوا۟ رَبَّنَآ أَخِّرْنَآ إِلَىٰٓ أَجَلٍۢ قَرِيبٍۢ نُّجِبْ دَعْوَتَكَ وَنَتَّبِعِ ٱلرُّسُلَ ۗ أَوَلَمْ تَكُونُوٓا۟ أَقْسَمْتُم مِّن قَبْلُ مَا لَكُم مِّن زَوَالٍۢ
Na waonye watu siku itapo wajia adhabu, na walio dhulumu waseme: Ewe Mola wetu Mlezi! Tuakhirishe muda kidogo tuitikie wito wako na tuwafuate Mitume. Kwani nyinyi si mliapa zamani kwamba hamtaondokewa?
وَسَكَنتُمْ فِى مَسَٰكِنِ ٱلَّذِينَ ظَلَمُوٓا۟ أَنفُسَهُمْ وَتَبَيَّنَ لَكُمْ كَيْفَ فَعَلْنَا بِهِمْ وَضَرَبْنَا لَكُمُ ٱلْأَمْثَالَ
Na mkakaa katika maskani zile zile za walio zidhulumu nafsi zao. Na ikakudhihirikieni jinsi tulivyo watendea. Nasi tukakupigieni mifano mingi.
وَقَدْ مَكَرُوا۟ مَكْرَهُمْ وَعِندَ ٱللَّهِ مَكْرُهُمْ وَإِن كَانَ مَكْرُهُمْ لِتَزُولَ مِنْهُ ٱلْجِبَالُ
Na kwa hakika walifanya vitimbi vyao, na vitimbi vyao anavijua Mwenyezi Mungu. Wala vitimbi vyao si vya kuondosha milima.
فَلَا تَحْسَبَنَّ ٱللَّهَ مُخْلِفَ وَعْدِهِۦ رُسُلَهُۥٓ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ عَزِيزٌۭ ذُو ٱنتِقَامٍۢ
Basi usimdhanie Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye kuwavunjia ahadi yake Mitume wake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda, na ni Mwenye kulipiza.
يَوْمَ تُبَدَّلُ ٱلْأَرْضُ غَيْرَ ٱلْأَرْضِ وَٱلسَّمَٰوَٰتُ ۖ وَبَرَزُوا۟ لِلَّهِ ٱلْوَٰحِدِ ٱلْقَهَّارِ
Siku itapo geuzwa ardhi iwe ardhi nyengine, na mbingu pia. Nao watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu Mmoja, Mwenye nguvu.
وَتَرَى ٱلْمُجْرِمِينَ يَوْمَئِذٍۢ مُّقَرَّنِينَ فِى ٱلْأَصْفَادِ
Na utaona wakhalifu siku hiyo wamefungwa katika minyororo;
سَرَابِيلُهُم مِّن قَطِرَانٍۢ وَتَغْشَىٰ وُجُوهَهُمُ ٱلنَّارُ
Nguo zao zitakuwa za lami, na Moto utazigubika nyuso zao.
لِيَجْزِىَ ٱللَّهُ كُلَّ نَفْسٍۢ مَّا كَسَبَتْ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ سَرِيعُ ٱلْحِسَابِ
Ili Mwenyezi Mungu ailipe kila nafsi kwa yale iliyo yachuma. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
هَٰذَا بَلَٰغٌۭ لِّلنَّاسِ وَلِيُنذَرُوا۟ بِهِۦ وَلِيَعْلَمُوٓا۟ أَنَّمَا هُوَ إِلَٰهٌۭ وَٰحِدٌۭ وَلِيَذَّكَّرَ أُو۟لُوا۟ ٱلْأَلْبَٰبِ
Hili ni Tangazo liwafikie watu, liwaonye, na wapate kujua kuwa hakika Yeye ni Mungu Mmoja, na wapate kukumbuka wenye akili.